Thursday, September 28, 2017

SEKTA YA MANUNUZI YA MTANDAONI NA CHANGAMOTO ZAKE NCHINI


Na Jumia Travel Tanzania

Miongoni mwa sekta ambazo zimewapatia utajiri mkubwa wafanyabiashara mbalimbali duniani ni pamoja na biashara kwa njia ya mtandao. Leo hii ukiyataja majina ya kampuni kama vile Alibaba au Amazon ni watu wachache wasioyafahamu licha ya kutokuwepo nchini Tanzania. Waasisi wa makampuni hayo wamo kwenye orodha ya watu matajiri duniani, Bw. Jeff Bezos mwasisi wa Amazon ni tajiri nambari 3 huku Jack Ma ambaye ni mwasisi wa Alibaba yeye ni tajiri nambari 23.

Utajiri wa wafanyabiashara hawa sio kama wanamiliki biashara katika nchi mbalimbali bali uwezo wa makampuni yao kuwafikia wateja mahali popote walipo. Kuwafikia wateja hao Jumia Travel ingependa kukufahamisha si kwa njia nyingine bali ni kupitia mtandao wa intaneti.

Kuja kwa mtandao wa intaneti kumerahisisha shughuli mbalimbali ikiwemo uendeshaji wa biashara. Mitandao kama Alibaba na Amazon iliona fursa kubwa kupitia intaneti ambazo inawezekana wafanyabiashara wenyewe hawakuziona. Fursa ambazo wao waliziona ni kwa kuwakutanisha wateja kutoka sehemu tofauti mtandaoni.

Hivyo wao suluhu waliyoiona badala ya wafanyabiashara kutegemea wateja kuja moja kwa moja dukani, wao waliona ni vema wafanyabiashara kuziweka bidhaa zao mtandaoni zikiwa na taarifa kamili kama vile mwonekano wake, sifa, ubora, bei na namna ya kuzipata. Baada ya kufanya hivyo ndipo wateja wao wenyewe wapitie mtandaoni na kuchagua zile walizovutiwa nazo.

Tafiti mbalimbali zilizofanywa na taasisi tofauti za kibiashara zimebaini kwamba kuna mambo ya msingi kadhaa ya kuzingatia pale unapotaka kufanya biashara kwa njia ya mtandao. Yapo masuala mbalimbali ambayo wafanyabiashara wanaaswa lakini yafuatayo ndiyo msingi mkuu zaidi.

Uharaka. Mojawapo ya changamoto kubwa ambayo manunuzi ya bidhaa mtandaoni imekuja kutatua ni upoteaji wa muda unaotumiwa na mteja kutoka eneo moja kwenda kwingine. Hivyo basi, ili kumshawishi mteja anunue bidhaa zako kwa mfumo huo lazima umhakikishie kwamba atatumia muda mchache mpaka kuipata huduma hiyo. Isiwe kwamba mteja anatumia muda mwingi kuipata bidhaa aliyoiagiza tofauti kama angeamua kuifuata mwenyewe dukani. Tafiti zinaonyesha kwamba wateja wapo tayari kulipa zaidi endapo kutakuwepo na uharaka mkubwa wa kufukiwa na huduma.

Uaminifu. Je bidhaa aliyoiona na kuiagiza mteja ndiyo sahihi iliyomfikia? Je sifa ambazo alizoziona mtandaoni ndizo anazoziona mara baada ya bidhaa kumfikia? Je ni kweli bidhaa imemfikia kwa wakati kama alivyoahidiwa baada ya kufanya manunuzi? Haya ni maswali ya msingi ambayo mteja wa mara ya kwanza wa mtandaoni atakuwa anasubiri majibu. Majibu ya maswali hayo ndiyo yatakayozaa uaminifu baina ya mfanyabiashara na mteja ili aendelee kufanya manunuzi tena na tena. Kama mfanyabiashara, uaminifu ni kitu muhimu sana kwani kumbuka ni mtandao pekee ndio unaowaunganisha.

Vifungashio (Packaging). Endapo ulikuwa haufahamu miongoni mwa vitu ambavyo huwavutia wateja ni pamoja na bidhaa inavyofungashwa. Hii inamaanisha kwamba vile bidhaa ungependa kumfungashia baada ya kufanya manunuzi kwa kuja dukani kwako iwe sawa ni vile itakavyokuwa kwa mtandaoni. Bila ya kujali mteja amemtumia kiasi gani kwenye manunuzi yake, vifungashio vya kuvutia humfanya kuridhika zaidi na kuvutiwa kutumia tena huduma zako.


Mbali na dunia kubadilika na kuhamia kwenye mifumo ya kimtandao bado kwa nchi zinazoendelea kama vile Tanzania ni changamoto. Baadhi ya sababu ambazo zimekuwa zikiwafanya watanzania kuwa wazito kidogo kufanya manunuzi ya bidhaa mtandaoni ni pamoja na:

Kuiona bidhaa. Ni utamaduni sio tu wa watanzania bali hata waafrika wengi pia kufanya maamuzi juu ya bidhaa wanayotaka kuinunua mpaka kuiona. Hivyo basi zinahitajika jitihada za ziada katika kuwaaminisha wateja kwamba kile wanachokiona ndicho watakachokipata.

Kuishika na kuijaribu bidhaa ili kujiridhisha. Kuiona tu bidhaa pekee haitoshi, watanzania wengi wana kawaida ya kuishika na hata kuijaribu bidhaa kabla ya kufanya maamuzi. Kwa kufanya hivyo wanaamini kwamba wanakuwa wamejiridhisha kwamba ni chaguo sahihi ndipo wafanye maamuzi. Kuitatua changamoto hii wafanyabiashara wanatakiwa kutoa elimu ya kutosha kwa wateja wao kuzifahamu kwa undani zaidi bidhaa wanazozihitaji ili kutokuwa na wasiwasi pale wanapofanya manunuzi.

Ugumu katika kuitumia tekinolojia. Kutokana na changamoto ya tekinolojia hizi mpya sio watu wana ufahamu wa kutosha wa namna ya kuzitumia. Elimu ya kutosha inahitajika pamoja juu ya mifumo na urahisi kwenye kuitumia. Ili manunuzi ya mtandaoni yawe rahisi basi kuna umuhimu wa mifumo kuwa rafiki kwa wateja.

Hofu ya wizi wa mitandaoni. Kwa kuwa mifumo hii ni mipya miongoni mwa watanzania wengi, bado kuna hofu juu ya tahadhari za wizi unaoweza kutokea mitandaoni. Wafanyabiashara wa mitandaoni wanatakiwa kuwaelimisha na kuwaaminisha kwamba ni salama. Mbali na hapo inabidi kubuni njia salama zaidi za malipo au kutumia ile mifumo ambayo watanzania wanaiamini kama vile kulipia bidhaa pale zinapowafikia.

Sababu ya mwisho ingawa zipo nyinginezo ni muda unaotumika mpaka bidhaa kumfikia mteja. Kuzingatia uharaka kwenye kuwafikishia wateja bidhaa pale walipo ndio kitu cha kuzingatia zaidi katika biashara za mtandaoni. Na nadhani ndio sababu kubwa iliyopelekea mfumo wa biashara kuenea sehemu nyingi duniani. Kwa mfano, Dar es Salaam ni miongoni mwa jiji yanayokumbwa na changamoto ya foleni za magari barabarani. Hali hiyo hupelekea wakazi wake kupoteza muda mwingi ambao ungeweza kutumika sehemu nyingine. Hivyo kwa kulitambua hili wafanyabiashara wa manunuzi ya mtandaoni wanaweza kuitumia kama fursa kwa kuwafikishia huduma wateja pale walipo huku wao wakiendelea na shughuli nyingine za kujenga taifa.

Ni dhahiri kwamba tekinolojia imedabili shughuli nyingi sana na kuwafanya kuwa werevu ukilinganisha na kipindi cha nyuma. Jumia Travel inaamini wafanyabishara hawana budi kuyazingatia mambo ya msingi katika uendeshaji wa biashara za mitandaoni na kuzijua tamaduni za watanzania. Kikubwa zaidi ni kuwajua wateja ni watu wa aina gani, wana mitazamo ipi na vitu gani wanapendelea ni mwanzo wa kufanikiwa kwenye jambo lolote.


No comments:

Post a Comment