Hususani kuhusu uondoaji wa wafanyakazi
hewa,
Sera ya elimu bure na usimamishwaji wa watumishi wa serikali kutokana na
makosa mbalimbali.
Lakini
wananchi hawakubaliani na kuzuiwa uagizwaji wa sukari kutoka nje pamoja na bei
elekezi ya sukari
15 Septemba 2016, Dar es Salaam: Uondoaji
wa wafanyakazi hewa ulitajwa na asilimia 69 ya wananchi wa Tanzania, kama
juhudi mojawapo ya Rais John Pombe Magufuli, wanayoifurahia sana. Elimu bure
(asilimia 67) na usimamishwaji wa watumishi wa serikali (asilimia 61) navyo pia
vilishika nafasi za juu. Walipoambiwa wataje vitendo ambavyo hawakubaliani
navyo, asilimia 32 walitaja kuzuiliwa kwa uagizwaji wa sukari na bei elekezi ya
sukari. Hatahivyo, asilimia 58 hawapingi kitendo chochote cha Rais. Kwa ujumla
kiwango cha kukubalika kwa Rais Magufuli anakubalika na asilimia 96 ya
wananchi. Kiwango hiki kinaendana na viwango vya kukubalika kwa marais wa
Tanzania waliopita.
Pamoja na hayo, asilimia 88 ya wananchi
wana imani kuwa Rais Magufuli ataendelea na kasi aliyoanza nayo, mpaka mwisho
wa awamu yake ya uongozi.
Viwango vya kukubalika vya viongozi
wengine wa serikali pia vipo juu Wananchi wanaonekana kumkubali
mwenyekiti wao wa kijiji/mtaa (asilimia 78), diwani wao (asilimia 74) na mbunge
wao (asilimia 68).
Matokeo haya yametolewa na Twaweza kwenye
utafiti uitwao Rais wa Watu? Tathmini na matarajio ya wananchi kwa serikali ya
awamu ya tano. Muhtasari huu unatokana na takwimu kutoka Sauti za Wananchi,
ambao ni utafiti wa kwanza barani Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa unaotumia
simu za mikononi. Matokeo haya yanatokana na takwimu zilizokusanywa kutoka kwa
wahojiwa 1,813 kutoka maeneo yote Tanzania Bara (Zanzibar haihusiki kwenye
matokeo haya) kati ya tarehe 4 Juni na tarehe 20 Juni 2016.
Wananchi wengi wanasema serikali ya
awamu ya tano imeleta maboresho kwenye huduma nyingi za umma. Inayoongoza ni
Mamlaka ya Mapato Tanzania ambapo asilimia 85 ya wananchi wanasema huduma
zimeboreshwa chini ya serikali mpya. Wananchi pia wanasema huduma ni nzuri
mashuleni (asilimia 75), vituo vya polisi (asilimia 74), mahakamani (asilimia
73), vituo vya afya (asilimia 72) na mamlaka za maji (asilimia 67). Ni vema
ikafahamika kuwa takwimu hizi zinaonyesha mitazamo na maoni ya wananchi kuhusu
huduma za umma na siyo lazima ikawa ndiyo hali halisi ya mabadiliko kwenye huduma
hizo. Vilevile, karibu wananchi wote (asilimia 95) wanasema watumishi wa umma
wanaotoa huduma, kama madaktari, walimu, pamoja na maofisa tawala wa umma
wamekuwa wakiwajibika zaidi.
Hata hivyo, wananchi wenyewe wanakubali
kuwa hawapati taarifa za kutosha kuhusu masuala muhimu ya kitaifa. Ni asilimia
4 tu wanaosema wanapata taarifa za kutosha kuhusu masuala ya siasa nchini na
asilimia 9 tu wanasema wanapata taarifa kuhusu masuala yanayohusu afya na
elimu. Hii inamaanisha kuwa maboresho yanayosemwa kuhusu huduma za umma
yanatokana na uzoefu binafsi au kutoka vyanzo visivyo rasmi. Hatahivyo,
wananchi wanatamani kupata taarifa kutoka katika sekta ambazo zinagusa maisha
yao. Walipoulizwa masuala gani wangependa kumuuliza mwenyekiti wao wa kijiji,
diwani au mbunge, masuala yanayohusu afya, elimu, maji na barabara yalijitokeza
kama mambo muhimu. Kwa upande wa Rais Magufuli, wananchi wawili kati ya kumi
(asilimia 18) wangependa kumuuliza kuhusu suala la mfumuko wa bei kwa bidhaa
mbali mbali.
Mwenendo unaofanana umejitokeza pale
wananchi walipoulizwa iwapo wanamfahamu au wameshazungumza na viongozi wao wa
vijiji, wilaya na kitaifa. Karibu wananchi wote (asilimia 96) waliripoti
kumfahamu Afisa Mtendaji wa Kijiji chao na karibu nusu yao (asilimia 47)
walikuwa wameshawahi kuzungumza naye. Hatahivyo, asilimia 21 ya wananchi
wanamfahamu Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya yao na asilimia 4 pekee wamezungumza
naye.
Pamoja na kiwango kikubwa cha kukubalika
kwa serikali ya awamu ya tano na Rais John Pombe Magufuli, wananchi wapo makini
na kanuni za demokrasia na haki na wanataka zifuatwe. Wananchi nane kati ya
kumi (au 80%) wanasema watendaji wa umma waondolewe pale tu panapokuwepo
udhibitisho wa vitendo viovu. Asilimia 75 wanasema kuwa watendaji waondolewe
pale wanaposhindwa kufanya kazi zao na siyo wanaposhindwa kufuata maagizo ya
Rais. Pamoja na shauku yao juu ya uondoaji wa watumishi wa umma, wananchi wana
maoni tofauti kuhusu matokeo ya kuwaondoa watumishi wa umma. Japokuwa asilimia
90 wanasema uondoaji wa watumishi hawa utawafanya watumishi wengine kuepuka
vitendo viovu, asilimia 37 wanasema itawapunguzia morali watumishi wengine.
Asilimia 48 wanasema uondoaji wa watumishi utawasababishia watumishi kutafuta
njia mpya za kuficha maovu.
“Wananchi wana mitazamo chanya kuhusu
utendaji wa serikali ya awamu ya tano pamoja na Rais Magufuli mwenyewe.
Wanasema kuwa watumishi wa umma kwenye maeneo mbalimbali wanawajibika zaidi na
kwamba wamegundua kuwa kuna maboresho kwenye huduma za umma. Hata hivyo
wananchi wana mashaka kuhusu utaratibu unaotakiwa kufuatwa. Kwa mfano, wanataka
udhibitisho wa vitendo viovu upatikane kwanza kabla ya watendaji kuwajibishwa,
kulaumiwa ama kutiwa aibu. Vilevile wana mashaka kuhusu maamuzi ambayo yanaweza
kugharimu fedha zao, kama kuzuia uingizwaji wa sukari. Hii inaonyesha kuwa
wananchi hawatakuwa wakikubaliana na vitendo vyote vinavyofanywa na Rais bila
kuhoji. Wananchi wanaendelea kuthamini misingi ya utawala bora
unaozingatia sharia zilizopo,’ anasema
Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze.
“Jambo muhimu kuhusu matokeo haya”
anaendelea Bwana Eyakuze, “ni kuwa matarajio ya wananchi yamebadilika.
Kipindi cha nyuma kulikuwa na hali ya kutokujali miongoni mwa wananchi, uzoefu
uliotokana na utendaji duni uliodidimiza matarajio yao, na matokeo yake
yakichangia utendaji usioridhisha kuendelea. Lakini mabadiliko tunayoyaona hivi
sasa yanaonyesha kuwa utendaji wa sekta ya umma unaweza kuimarika. Wananchi
wanaweza kutarajia viwango vya juu zaidi kama utaratibu huu mpya ni wa kudumu.”

No comments:
Post a Comment