Monday, May 30, 2016

RC MWANZA AWATAKA WAFANYABIASHARA KUWEKEZA KATIKA KUJENGA SHULE

Na Jovin Mihambi,Mwanza

MKUU wa Mkoa wa Mwanza Bw John Mongella (Pichani Kulia) amewataka wafanyabiashara mkoani humo kuwekeza katika sekta ya elimu ambayo bado ina uhitaji mwingi na shule hizo zielekezwe katika mchepuo wa masomo ya sayansi ili serikali iweze kupata wataalamu wengi kuliko kutegemea wale kutoka nje.

Aliyasema hayo juzi (Jumapili) katika hotuba yake kwa wahitimu wa kidato cha sita katika shule ya Alliance International Schools and Sports Academy yaliyofanyika shuleni hapo, kata ya Mahina  jijini hapa.

Alisema kuwa wafanyabiashara hao wakijenga shule hususani za sekondari zenye mchepuo wa sayansi serikali itaweza kukidhi haja yake ya kupata wataalamu wenye fani zinazoendana na masomo ya sayansi tofauti na ilivyo kwa sasa ambapo wataalamu wengi ni kutoka nje ya nchi.

Alisema kuwa kwa upande wa wataalamu hususani upande wa afya, serikali itaweza kuwa na wataalamu wengi kwa upande wa tiba na itaondokana na kupeleka wagonjwa nje kwa ajili ya upasuaji na magonjwa mengine.

Bw Mongella alipongeza uongozi wa shule ya Alliance Schools and Sports Academy kwa kuanzisha shule ya sekondari kidato cha tano na sita katika mchepuo wa sayansi na kuongeza kuwa utaratibu huo unakidhi kiu ya serikali ya kutaka kujenga shule za sekondari nyingi nchini zenye mchepuo wa sayansi.

"Pia, mwanafunzi anapochukua masomo ya sayansi, anakuwa na uhakika anapoingia chuoni na kuendeleza fani hiyo, huweza kupata kazi kwa urahisi kuliko fani zingine ambazo wahitimu huangaika kutafuta kazi ambazo hazipatikani kwa urahisi", alisema Mongella.

Kuhusu utumbuaji majipu ambayo yanafanywa na serikali ya awamu ya tano, alisema kuwa hiyo ni sahihi kutokana kwamba baadhi ya watendaji serikalini walikuwa wamejisahau na kufanya mambo ndivyo sivyo.


"Serikali ya awamu ya tano haina muda wa kupoteza kwa sababu tuko nyuma sana hususani kutowashughulikiwa walaji rushwa na vitendo vingine vya ufisadi na hatuna mda wa kuunda tume. Ukionekana umeboronga sehemu fulani utatumbuliwa", alisema Mongella.

Naye Mkurugenzi wa Shule za Alliance Schools and Sports Academy Bw James Bwire, alisema kuwa hapo mwakani, matarajio ya shule yake ni kufungua chuo cha ualimu kuanzia ngazi ya cheti hadi stashahada ili kukidhi mahitaji ya taifa na atatoa kipaumbele kwa wanachuo ambao watasomea masomo ya sayansi.



No comments:

Post a Comment