Thursday, February 18, 2016

PROFESA MBARAWA AWASIMAMISHA NA KUWASTAAFISHA BAADHI YA WAKURUGENZI TCRA

Na Benedict Liwenga-MAELEZO.
WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Profesa Makame Mbarawa amewasimamisha na kuwastaafisha kwa manufaa ya Umma baadhi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania.

Taarifa hiyo ameitoa leo ofisini kwake Jijini Dar es Salaam mara alipokutana na Waandishi wa Habari ambapo ameeleza kuwa, hatua hiyo imetokana na kutofungwa kwa kifaa kinachowezesha mtambo wa kufuatilia Mapato ya Simu (TTMS) hali iliyopelekea Mamlaka ya Mawasiliano na Mamlaka ya Kodi kushindwa kubaini mapato halisi ya makampuni ya simu na hivyo kushindwa kukokotoa kodi stahiki zinazotakiwa kulipwa na makampuni ya simu nchini na kuikosesha Serikali mapato ya kiasi cha shilingi bilioni 400 pesa za kitanzania.

Akieleza kuhusu kazi za mtambo huo, Profesa Mbarawa amesema kuwa, mtambo ulitakiwa uwe na uwezo wa kufanya kazi ya kuhakiki ubora wa huduma za mawasiliano, kutoa Takwimu za mawasiliano yanayofanyika ndani na nje ya nchi, kutambua mapato na miamala ya fedha mtandao, kufuatilia na kugundua mawasiliano ya ulaghai, kutambua taarifa za laini ya simu na za kifaa cha mawasiliano pamoja na mapato ya simu za ndani.

‘’Kwa kushindwa kutoa ushauri wa Kisheria na kitaalamu, kwa uzembe au kwa manufaa yao binafsi, Mkurugezni wa Idara ya Sheria Bi. Elizabeth Nzagi na wasaidizi wao akiwemo Kaimu Mkurugenzi anayesimamia Mtambo wa Kuchunguza Mapato katika Mitandao ya Simu (TTMS) Injia Sunday Richard na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sheria Bw. Modestus Ndunguru wamesabbisha mtambo huo kufuatilia mapato ya simu kutoka nje ya nchi pekee na kutofungwa kifaa kinachowezehsa mtambo huo kufuatilia mapato ya simu za ndani,’’alisema Profesa Mbarawa.

Aidha, Profesa Mbarawa ameiagiza Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kusitisha mara moja Mkataba wa Mkurugenzi wa Idara ya Sheria Bi. Elizabeth Nzagi ambapo pia ameigaiza Bodi hiyo kuwasimamisha kazi mara moja Kaimu Mkurugenzi anayesimamia Mfumo wa kuhakiki na kusimamia huduma za Mawasiliano (TTMS) Injinia Sunday Richard na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sheria Bw. Modestus Ndunguru ili kupisha uchunguzi dhidi ya uhusika wao katika kusababisha kutofungwa kwa kifaa kinachowezesha mtambo wa kufuatilia Mapato ya Simu (TTMS) ili kufuatilia mapato ya simu za ndani ya nchi.

Profesa Mbarawa pia ametoa onyo kali kwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania Dkt. Ally Simba kwa kutokuwa makini na utendaji wake mpaka kupelekea kutokea kwa hali hiyo na kuhakikisha kuwa tabia hiyo haijirudii tena.

‘’Namwagiza Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Dkt. Ally Simba kuhakikisha kuwa, ndani ya siku saba, Kampuni iliyofunga mtambo huo inafunga kifaa hicho kinachotambua mapato ya simu za ndani, naielekeza TAKUKURU kufanya uchunguzi wa kina tangu mtambo ulipofungwa na utaratibu mzima uliotumika kuipata Kampuni iliyofanya kazi hiyo,’’aliongeza Profesa Mbarawa.

Mnamo tarehe 22 Machi mwaka 2013 Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) iliingia Mkataba na Kampuni ya Consortium of Societe Generale de Surbveillance SA (SGS) na Global Voice Group (GVG).








No comments:

Post a Comment