Monday, June 09, 2014

MAAJABU YA SAYANSI: MATUNDA SASA KUPRINTIWA BADALA YA KULIMWA SHAMBANI

Jiandae kushuhudia mapinduzi makubwa ya sayansi na teknolojia duniani, kuhusiana na uchapishaji wa chakula badala ya kuotesha shambani sasa kwa kutumia printer utaweza kuchapisha chakula chenye ladha kamili.

Kampuni moja iliyoko nchini Uingereza imetengeneza printer ya 3D ambayo itaweza kuchapisha matunda. Printer hiyo inatumia teknolojia ya Molecular-gastronomy inayoitwa “spherification” huchanganya majimaji pamoja na ladha kutengeneza umbile la tunda lenye ladha.

Wengi wetu tumezoea chombo cha kuchapisha maandishi, picha nakadhalika kutoka kwenye kompyuta, sasa wanasayansi wamekwenda hatua kubwa zaidi na kutengeneza chombo kama hicho chenye teknolojia yenye mielekeo mitatu (3D) ili kuchapisha vyakula.
Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa katika mtandao wa NDTV Cooks, mwishoni mwa wiki iliyopita, ni kwamba mtu haitaji kuwa mtaalamu ili kutumia printer hiyo. Matokeo ya kinachotolewa na mashine hiyo ni tunda ambalo lina uhalisia.
Shirika la habari la AP (Associated Press) lilimkariri mbunifu wa chombo hicho, Vaiva Kalnikaite “Printer yetu ya matunda italeta uwezekano mpya, sio tu kwa wapishi mahotelini, lakini pia kwa wapishi nyumbani, kwa kuturuhusu na kutupa fursa ya kuboresha uzoefu wetu jikoni.”
Kalnikaite anasema kuwa “tumebadilisha namna ya kukidhi mahitaji ya watumiaji na walaji wa matunda.”
Mbunifu mwenzie kutoka Dovetailed, Gabriel Villar anasema kwa ubunifu huu wa kipekee, sio tu utaweza kuchapisha matunda yako mwenyewe, bali pia utaweza kubuni tunda la aina yako mwenyewe kwa mahitaji yako binafsi”

Chakufurahisha ni kwamba, hii siyo mara ya kwanza kusikia printer ya 3D ya chakula. Kampuni moja kutoka Spain ilishatoka na teknolojia kama hiyo inayochapisha chakula iliyozinduliwa mwaka jana.
Kampuni hiyo iliyoko katika jiji la Barcelona, Natural Machines ilitengeneza printer ya chakula na kuiita “Foodini” wanadai kuwa mashine hiyo inachanganya “teknolojia, chakula , sanaa na ubunifu”
Kama haitoshi huko Marekani, kampuni iliyoko Carolina Kusini ijulikanayo kama 3D Systems Inc. pia ilizindua Chefjet Pro, ikiwa ndio teknolojia ya kwanza ya kuchapisha chakula.


No comments:

Post a Comment