Wednesday, March 05, 2014
ASHAMBULIWA NA KIBOKO NA KUUAWA
BUNDA.
Mwanaume mmoja, Mukoba Juma mkazi wa Kijiji cha Guta B wilayani Bunda mkoani Mara ameshambuliwa na kuuawa na Kiboko katika ufukwe wa Ziwa Victoria wakati akifanya shughuli za uvuvi.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Guta B, Kisheri Nyihande amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa juzi saa 12 jioni marehemu pamoja na rafiki yake aliyemtambulisha kwa jina moja la Madege walienda kuvua katika ziwa Victoria kwa lengo la kupata kitoweo.
Nyihande alisema wakiwa katika shughuli hiyo ghafla alijitokeza mnyama huyo na aliyemrusha marehemu ndani ya maji huku yeye Madege akitimua mbio kunusuru maisha yake.
Alifafanua kuwa Madege alipiga kelele kitendo kilichowafanya wananchi kufika katika eneo la tukio na kuanza kuutafuta mwili wa marehemu ambao hata hivyo ulipatikana jana saa tatu asubuhi ukiwa na majeraha makubwa na mwili huo kuzikwa jana saa 10 jioni.
Wakiwa katika eneo la mazishi huku wakiwa na majonzi mengi wananchi wakiungana na familia ya marehemu waliomba serikali kupitia kitengo cha mali asili kuweka mkakati wa kudumu wa kufanya doria katika maeneo hayo ili kunusuru maisha ya wananchi hao.
Mtendaji wa Kijiji hicho Reymond Misana alisema tayari katika siku za hivi karibuni wakazi watatu wa kijiji hicho wamepoteza maisha kwa kushambuliwa na wanyama hao hasa Mamba na Kiboko na wengine kupata ulemavu.
Aidha alisema fidia au kifuta jasho kwa familia zinazoathiriwa na wanyama hao imekuwa kitendawiili licha ya serikali ya kijiji kuwasilisha malalamiko hayo kwa idara ya mali asili wilayani Bunda.
Jeshi la polisi wilayani Bunda imethibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment