Sunday, December 22, 2013

BREAKING NEWS:RUNDO LA SHABA ZA WIZI LAKAMATWA

File picture
Mwanga

HALMASHAURI ya wilaya ya Mwanga imefanikiwa kuokoa tani zaidi ya 100 za shaba zilizochimbwa kinyemela na kutaka kusafirishwa kusikojulikana huku ikikadiriwa kuwepo kwa tani zaidi ya 280 za shaba zilizotoroshwa.

Taarifa hiyo ikiwa ni baada ya madiwani wa halmashauri hiyo kulalamikia uvamizi unaofanywa na baadhi ya watu kwa madai ya kufanya utafiti wa uwepo wa madini katika maeneo mbalimbali ambapo pia walitaka orodha ya maeneo ya wilaya hiyo yanayochimbwa madini.

Akizungumzia hali hiyo, mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Leti Shuma alisema madini hayo yamezuiliwa katika eneo la Chang’ombe kijiji cha VuchamaNdambwe ikiwa ni baada ya kugundulika kuwepo kwa wachimbaji wadogo kinyume cha taratibu.

Alisema eneo hilo la uchimbaji awali lilikuwa na mgogoro ambao uliisha baada ya mkataba wa mwekezaji wa awali kuisha ambapo baadaye kuliibuka wimbi la watu walikuwa wakichimba shaba katika eneo hilo bila kufuata utaratibu.

Shuma alisema madini hayo tani 100 zinalindwa na halmashauri katika eneo hilo zikimsubiria mwekezaji halali wa eneo hilo kampuni ya Zhong Tan ya nchini China ambaye anamkataba wa kuchimba madini katika eneo hilo wa miaka 10 ambaye bado hajaanza shughuli za uchimbaji.

“mkataba wake umesainiwa Februari 13 2012 na utaishia Februari 12 mwaka 2022 ambaye bado hajaanza shughuli za uchimbaji, kazi hiyo hufanywa na wachimbaji wadogo kinyume cha sheria shughuli ambazo zimesimamishwa na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya”alisema

Akitaja maeneo yanayo chimbwa madini katika wilaya hiyo, mkurugenzi alitaja kijiji cha VuchamaNdambwe madini ya shaba, kata ya Kirya, Gypsum na madini ya mchanga ambayo huchimbwa maeneo tofauti ya wilaya hiyo kwenye mashamba ya watu binafsi.

Ufafanuzi huo wa mkurugenzi umekuja ikiwa ni baada ya madiwani kutaka orodha ya maeneo yanayochimbwa madini katika wilaya hiyo pamoja na kutaka kujua hatima ya madini ya shaba tani 100 ambazo zinashikiliwa katika eneo hilo.

Katika hoja yake diwani wa kata ya Kisangara, Mamboleo Teri alitaka utafiti wa kina kufanyika ili kujua maeneo halisi yanachimbwa madini kwani wilaya hiyo inayomengi ikilinganishwa nay ale yanayotajwa kila wakati katika taarifa mbalimbali.

Aidha diwani huyo aliitaka halmashauri hiyo kuandaa mpango maalum wa kuhakikisha wawekezaji katika sekta ya madini wa nazinufaisha jamii zinazo wazunguka ili kuepusha migogoro inayoweza kujitokeza.

“mpango huo maalum uwe ni utaratibu wa wilaya yetu kila mwekezaji anayeingia apewe, lakini pia saidieni vijiji kutunga sheria ndogo ndogo zitakazowawezesha kupata ushuru kwa hawa wachimbaji wa madini tofauti na hali ilivyo sasa”alisema

No comments:

Post a Comment