Wednesday, July 17, 2013

WANANCHI TUSHIRIKIANE KATIKA KUZUIA UJANGILI


Wizara ya Maliasili na Utalii inawajulisha wananchi kuwa ingawaje kumekuwa na taarifa za kuongezeka kwa ujangili nchini na hasa mauaji ya kinyama ya tembo na usafirishaji haramu wa wanyama hai na meno ya tembo.

Wizara inajitahidi sana kupambana na uhalifu huu kulingana na watumishi waliopo na fedha na vitendea kazi vilivyopo. Kwa mfano, mwaka 2012/13 pekee (kufikia Machi 2013) watuhumiwa 1,215 walikamatwa kwa makosa mbalimbali wakiwa na jumla ya bunduki 85 na risasi 215 za aina mbalimbali.


Kesi 670 zilifunguliwa katika mahakama mbalimbali nchini. Kati ya hizo, kesi 272 zimemalizika kwa washitakiwa 247 kulipa faini ya jumla ya shilingi 175,002,420/= na washitakiwa 71 kupewa adhabu ya vifungo vya jumla ya miaka 99. Aidha, kesi 398 zenye jumla ya washitakiwa 897 bado zinaendelea katika mahakama mbalimbali nchini.

Vita dhidi ya ujangili ni ngumu hasa ukizingatia kuwa, baadhi ya Watanzania wanaamini kuwa jukumu hili ni la serikali pekee na hasa maafisa na askari wanyamapori. Dhana hii ni potofu kwani, uzuiaji ujangili kamwe hautafanikiwa kama wananchi na wadau wengine walioko ndani na nje ya nchi yetu wataendelea kubakia watazamaji tu.

Wizara inaomba sote tuitafakari na kuitekeleza dhana ya Jeshi la Polisi ya Ulinzi Shirikishi. Ni muhimu kila mwananchi mzalendo wa nchi hii ashiriki kikamilifu kudumisha amani na ulinzi wa nchi na rasilimali zake zote. Hivyo basi, wananchi wanaweza kutoa taarifa za kina na uhakika zitakazopelekea kukamatwa majangili na/au wafadhili wao.

Yeyote mwenye taarifa azitoe ama kwa Afisa Wanyamapori aliye karibu yake, Makao Makuu ya Idara ya Wanyamapori, TANAPA, Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro au Kituo cha Polisi kilichokaribu.

Aidha, ikumbukwe kuwa hapa nchini, zaidi ya asilimia 90 utalii unategemea wanyamapori. Watalii wengi huja kuwaona, kuwapiga picha na kuondoka. Wachache huja kuwawinda kisheria na kuchukua nyara. Wanyamapori ndio wamebeba utalii katika Tanzania na kwa maana hiyo ndio, kwa kiasi kikubwa, wamebeba uchumi wa nchi hii – ndio wanatununulia dawa, vitabu mashuleni na kutujengea barabara.

Wizara inatoa wito kwa Watanzania kuwa tuache kumtazama fisi kama mnyama mwenye sura mbaya na anayenuka; na tuache kumtazama tembo kama kero kwa wakulima na kwa hiyo kufurahia kuuawa kwao. Badala yake tuwatazame wanyamapori kama benki kubwa na kama mkombozi wa nchi yetu kiuchumi.

Wanyamapori kama ilivyo viumbe hai, huzaliana. Hivyo, kama tutashirikiana kuwalinda na kuwatumia kiendelevu si miaka mingi tangu sasa watakuwa namba moja katika kuchangia pato la Taifa letu.



No comments:

Post a Comment