Wednesday, April 17, 2013
HUYU NDIYE BI. KIDUDE
FATMA binti Baraka, maarufu kwa jina la Bi Kidude, ni miongoni mwa wasanii wanawake wachache ambao ni magwiji wa muziki wa taarabu nchini, ni mzaliwa wa Zanzibar lakini asili ya kabila lake ni Mmanyema kutoka Mkoa wa Kigoma, magharibi mwa nchi.(113)
Bi. Kidude aliweza kuteka soko la muziki hususani wa mwambao kwa kutunga mashahiri yaliyobeba ujumbe wa mahaba pamoja na mafumbo kwa lugha ya kiswahili yenye lengo la kufikisha ujumbe wake kwa mashabiki wake
Muimbaji huyo aliweza kutamba na vibao mbalimbali ikiwemo Yalait ,Muhogo wa Jang’ombe, Kijiti, Arebaba na Machozi ya huba na nyinginezo ni nyimbo ambazo zilizojizolea umaarufu katika soko la muziki wa taaarabu
Mkongwe huyu wa taarabu nchini, ambaye amejizolea umaarufu kupitia tasnia hiyo katika maisha yake hajabahatika kupata mtoto ingawa aliwahi kuolewa mara mbili
Kwa mujibu wa mahojiano mbalimbali aliyofanya na vyombo tofauti tofauti vya habari Bi. Kidude alielezea asili la jina lake kuwa alipewa na mjomba wake wakati alipozaliwa kwa sababu alikuwa na umbile dogo.
Mkongwe huyo wa muziki amekuwa muimbaji tangu miaka ya 1920 akiwa ni mfuasi wa Sitti Bin Saad mmojawapo wa waimbaji wa mwanzo kabisa wa taarabu visiwani Zanzibar.
Akiwa na umri wa miaka 13 hakuwa na jinsi bali kukimbilia Tanzania bara(Tanganyika enzi hizo) ili kuepuka kuozeshwa kwa nguvu. Akiwa Tanzania bara alizunguka kila kona ya nchi akiwa muimbaji katika makundi mbalimbali ya muziki wa taarabu likiwemo lile maarufu la Egyptian Musical Taarab. Baadaye alihamia nchini Misri kwa kifupi kabla hajarejea kisiwani Zanzibar mahali ambapo umauti wake ulipomkuta.
Tuzo alizowahi kupokea Bi. Kidude ikiwemo mwaka 2005 , nchini Uingereza,ambapo alipokea tuzo yenye heshima kutoka World Music Expo (WOMEX) kwa mchango wake katika muziki na utamaduni wa Zanzibar. Katika kinyang’anyiro hicho aliwashinda wanamuziki mahiri kama Peter Gabriel, Miriam Makeba na wengineo.
Mwaka jana, kampuni ya nchini Uingereza iitwayo ScreenStation kwa kushirikiana na Busara Promotions walitoa documentary iitwayo “As Old As My Tongue-The Myth and Life of Bi.Kidude” inayoelezea historia nzima ya maisha yake. Unaweza kuona dakika kama saba hivi za documentary hiyo hapa chini.Anasema yeye anakunywa na pia anavuta,lakini zaidi ya yote anaweza kuimba bila hata kutumia spika ya mdomo yaani microphone.
Pamoja na hayo katika mahojiano mbalimbali ambayo aliwahi kufanya muimbaji huyo alibainisha mtu wa kwanza kuthamini kazi za kumtafuta hadi kufika alipo alikuwa Rais mstaafu wa Tanzania wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi.
Anasema alipokuwa Rais wa Zanzibar, aliwaomba watu wamtafute Bi Kidude ili apate kumwimbia nyimbo za Siti, kwa kuwa hakuna aliyeweza kuziba pengo japo kidogo la Siti binti Saad.
Kama hiyo haitoshi, Bi kidude aliweza kufanya ziara mbalimbali kupitia muziki wake wa taarabu ambapo alijikuta hadi nchini Uingereza kwa Malkia Elizabeth II , ambapo alishuhudia sura ya picha yake ikiwa ndani ya kitabu cha malkia huyo na ndipo alipokabidhiwa kidani cha dhahabu
Hali hiyo ni heshima kubwa kwa mwanamuziki mkongwe huyo kukabidhiwa kidani cha dhahabu na malkia kutokana na hali hiyo Bi. Kidude ni miongoni mwa wasanii wa kwanza kutangaza nchi kupitia kazi ya muziki
Mbali na hayo muimbaji huyo alipelekwa kwa mara ya kwanza nchini Ujerumani na Mariam Hamdani, aliyemtambulisha kwa watu mbalimbali ambapo aliweza kusimama kwenye majukwaa na kutumbuiza.
Kutokana na umahili wa uimbaji wake pamoja na kuwa na mashahili yenye ubunifu huku akikitangaza kiswahili aliweza kuishi nchini Ajipshini (Egyptian) kwa miaka tisa kutokana na kazi hiyo ya muziki
Pamoja na hayo ameweza kuwa mmoja wa wasanii waliohudhuria uzinduzi wa kampeni ya Malaria iliyokwenda kwa jina la 'Zinduka' kwa kuhudhuria kampeni hiyo aliweza kukonga nyoyo ya Rais Kikwete
Moja ya sifa ya uimbaji wa mkongwe huyo wa taarabu na muziki wa mwambao ni kuwa na kipaji na ubunifu katika kazi zake huku, katika moja ya mahojiano yake aliweza kueleza kuwa muimbaji mzuri ni yule anayetumia kichwa na dhati ya moyo wake kwenye kuimba kwani kubana au kuibadili sauti wakati wa kuimba si sahihi, inamtoa mwimbaji kwenye uhalisia wake.
Mbali na hilo pia Bi. Kidude aliweza kuimba ingawa alikuwa mzee hivyo aliweza kutumia kipaji chake kwa ustadi mkubwa kwa kuwa mbunifu na kukiendeleza kwa kipindi chote cha uhai wake tofauti na baadhi ya wasanii wa sasa ambao wanasikika kwa kipindi kifupi baadae wanapotea kwenye fani ya muziki
Ingawa baadhi ya wasanii wengi wanaamini kuwa uvutaji wa sigara unachangia kumaliza sauti hali ilikuwa tofauti kwa muimbaji huyo ambaye hakuacha kuvuta sigara na badala yake kuwa shuhuda kwamba ameanza kuvuta sigara akiwa kijana na sauti yake haina mabadiliko
Kupitia mahojiano mbalimbali Bi. Kidude aliweza kuweka wazi kuwa alianza kuvuta sigara kwa muda mrefu na kutaja aina ya sigara ambazo aliwahi kuvuta ikiwemo na Seven , Mkasi, Simba, Kulindondo, Gundufleki na sasa Embassy ambapo ana uwezo wa kumaliza pakiti moja kwa siku tatu.
Mbali na kuwa mahili kwenye uimbaji pia alikuwa na uwezi wa kupiga ngoma baada ya kujifunza kwenye majahazi wakati akiwa na umri mdogo
Bi. Kidude alianza kuumwa mwishoni mwa mwaka jana akiwa akisumbuliwa na maradhi ya sukari, ambayo ni maradhi yake ya muda mrefu ila yalizidi baada ya kukiuka taratibu za vyakula
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment