Monday, October 02, 2017

WAJUMBE WA ALAT WAMLILIA RAIS MAGUFULI KUPATA MAJIBU YA CHANGAMOTO ZAO

PICHANI: Mwenyekiti wa ALAT Taifa Gulamhafeez Muccadam akifungua Mkutano Mkuu wa 33 utakaofanyika kuanzia Oktoba 2 hadi 5 kwenye Ukumbi wa J.K. Nyerere jijini Dar es Salaam. (Picha na Yusuph Mussa).

Na Yusuph Mussa

BAADHI ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa 33 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) wanamsubiri kwa shauku kubwa Rais Dkt. John Magufuli kufungua mkutano wa ALAT Taifa leo (Okt. 3).

Na hiyo ni kutokana na changamoto nyingi zinazozikabili halmashauri nyingi nchini ikiwemo posho ndogo wanazolipwa madiwani na fedha za miradi ya maendeleo na ruzuku ya matumizi ya kawaida kutoka Serikali Kuu kwenda halmashauri kuchelewa ama kutopelekwa kabisa.

Hayo yalisemwa jana (Okt. 2) na Meya wa Jiji la Dar es Salaam Chacha Mwita kwenye siku ya kwanza ya Mkutano Mkuu wa ALAT Taifa unaofanyika Ukumbi wa J.K. Nyerere International Convention Centre jijini Dar es Salaam.

Mwita alisema mameya na wenyeviti wa halmashauri wamekuwa wakiwekwa kitimoto na madiwani kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo posho zao kuwa ndogo, lakini hilo limewafanya wakose majibu, lakini kwa ujio wa Rais kwenye mkutano huo,wanaweza kupata majibu muafaka juu ya changamoto hizo.

"Ujio wa Rais kwenye ALAT kesho (leo) unaweza kuwa mwarobaini wa changamoto kwenye halmashauri, kwani madiwani wamekuwa wakiwakaba koo wenyeviti kuhusu posho zao. Hivyo tunaamini jambo hilo na mengine yote yatapatiwa majibu sahihi" alisema Mwita.

PICHANI: Wajumbe wa ALAT Taifa kutoka mkoa wa Tanga wakiongozwa na Mbunge wa Jimbo la Korogwe Vijijini Stephen Ngonyani 'Profesa Majimarefu' (kulia).

Akifungua mkutano huo, Mwenyekiti wa ALAT Taifa Gulamhafeez Muccadam alisema mambo yanayofanywa na Rais Dkt. John Magufuli ni lazima yaungwe mkono na Watanzania wote, kwani Rais ana nia njema kuona wananchi wanapata maendeleo.

"Mabadiliko yanayofanywa na Rais Dkt. John Magufuli yaungwe mkono, kwani yana tija, ufanisi na kuleta maendeleo. Hivyo wananchi na viongozi wa ngazi mbalimbali wanatakiwa kumsaidia ili kufikia malengo ya nchi ya viwanda na uchumi wa kati ifikapo 2025" alisema Muccadam.

Uchunguzi wa gazeti la Majira, umebaini changamoto nyingine kubwa ni halmashauri kushindwa kurejeshewa fedha zao kutokana na vyanzo vya mapato ya ndani vilivyofutwa, lakini na Serikali Kuu kupitia TRA, kukusanya mapato ya kodi ya majengo badala ya halmashauri, jambo hilo limepunguza mapato kwenye halmashauri hizo.

No comments:

Post a Comment