Na Mwandishi Wetu, Ruvuma
UONGOZI wa shamba la kahawa la Aviv lililopo Songea, mkoani Ruvuma, umesema upo mbioni kupunguza gharama za uzalishaji zao hilo baada ya kukamilika mradi mkubwa wa umeme 220 kV kutoka Makambako hadi Ruvuma.
Mradi huo ambao utahusisha vituo vitatu vya kupoozea umeme wa 220/33kV, unatarajiwa kukamilika Septemba 16,2018. Meneja wa shamba hilo, Hamza Kassim (Pichani), aliyasema hayo Mjini Songea, mkoani Ruvuma jana alipozungumza na Wahariri wa vyombo vya habari waliotembelea shamba hilo.
Alisema shamba hilo lililopo eneo la Lipokela kwa sasa linafanya uzalishaji kwa kutumia jenereta inayotumia mafuta lita 400 kwa siku. "Baada ya kukamilika mradi wa 220 kV kutoka Makambako hadi Songea, utatusaidia kupunguza gharama za uzalishaji kwa asilimia 70.
Aliongeza kuwa, umeme ambao wataunganishiwa kupitia mradi huo utaongeza shughuli za uzalishaji shambani na gharama walizopunguza zitatumika kutatua changamoto za wafanyakazi. Kassim alisema kwa sasa shamba hilo ambalo lilianzishwa mwaka 2011, limetoa ajira za kudumu kwa wafanyakazi 200, pia kinatoa ajira 300 hadi 350 kwenye msimu wa kuchuma kahawa.
Shamba hilo lina ukubwa wa hekta 1,012 ambazo wamezigawa maeneo matatu, kati ya hizo, hekta 800 zimekomaa zikiwa tayari kwa kuvunjwa na hekta zilizobaki ni kahawa mbichi.
"Kutokana na ukubwa wa shamba hili matumizi yetu ya umeme ni megawati 2.25 hadi 2.5 hivyo baada ya mradi kukamilika, uzalishaji unaweza kuongezeka na kutoa fursa nyingi za ajira kwa wafanyakazi," alifafanua Kassim.
Kwa upande wake, Meneja wa TANESCO mkoani humo, Mhandisi Patrick Lwesya alisema shamba hilo ni mteja mkubwa kuliko wawekezaji wote waliowekeza katika mji huo ambalo litapata Umeme kupiia mradi wa 220/33 kV.
"AVIV ni mdau wetu muhimu, anatumia umeme mwingi ambao ni megawati 2.25 hadi 2.5, hitaji la umeme Songea nzima ni megawati 5.35 hivyo ni wazi AVIV ni mteja muhimu," alisema.
No comments:
Post a Comment