Na Mwandishi Wetu, Mtwara
TATIZO la kukatika kwa umeme kwenye mikoa ya Mtwara-Lindi, linatokana na hitilafu iliyojitokeza katika mitambo minne kati ya tisa inayotumika kufua umeme kwenye kituo uzalishaji kilichopo mkoni Mtwara.
Tatizo hilo lipo mbioni kupatiwa ufumbuzi na mafundi wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO), ambao wameanza kufanya matengenezo katika mitambo hiyo kwa saa 24 (usiku na mchana). Naibu Mkurugenzi Mtendaji Usafirishaji Umeme kutoka Makao Makuu ya shirika hilo, Mhandisi Kahitwa Bishaija, aliyasema hayo Mjini Mtwara jana wakati akizungumza na Wahariri wa vyombo vya habari nchini.
Wahariri hao wapo katika ziara ya kutembelea miradi mbalimbali ya umeme inayotekelezwa na Serikali kupitia TANESCO kwenye mikoa ya Njombe, Ruvuma, Mtwara na Lindi. Alisema mafundi wa TANESCO walianza kufanya matengenezo ya mitambo mmoja, wakati kazi hiyo ikiendelea, mitambo mingine mitatu ilizima ghafra, kusababisha upungufu wa umeme unaozalishwa.
"Mitambo hii kila baada ya muda inahitaji kufanyiwa matengenezo, wakati mafundi wetu wakiwa katika kazi hiyo, mitambo mingine mitatu ilizima ghafra," alisema. Mhandisi Bishaija alisema ili kuhakikisha hali ya upatikanaji umeme kwenye mikoa hiyo inarudi kama ilivyokuwa awali, Serikali na TANESCO wamejipanga kuhakikisha tatizo lililopo linapatiwa ufumbuzi wa haraka.
Alisisitiza kuwa, lengo la Serikali ni kuhakikisha wateja wa TANESCO wanapatiwa umeme wa uhakika ili wautunie kwa shughuli zao za maendeleo na kujiingizia kupato.
Kwa upande wake, Meneja wa TANESCO Kanda ya Kusini, Mhandisi Aziz Salum, alisema kutuo cha Mtwara (Mtwara Power Plant), kinafua umeme wa laini 10 na kulisha mikoa ya Mtwara na Lindi.
"Kituo hiki kinafua umeme kwa kutumia gesi asilia na kilianzishwa Machi,2007...kituo kina uwezo wa kuzalisha umeme wa megawati 18, mpango wetu ni kuongeza megawati ili zifikie 22," alifafanua.
Alisema lengo la Serikali na TANESCO ni kujenga kituo kikubwa mkoani Mtwara ambacho kitazalisha umeme wa megawati 300 ili tatizo la kukatika kwa umeme liwe historia.
Mhandisi Salum alisema ongezeko la matumizi ya umeme kwa wateja katika mikoa hiyo ni matokeo ya kukua kwa shughuli za uzalishaji. Alitoa wito kwa wananchi kuona umuhimu wa kuilinda miundombinu ya TANESCO ambayo inanunuliwa kwa gharama kubwa.
No comments:
Post a Comment