Saturday, October 28, 2017
KATIBU MKUU KITILA AZINDUA JUKWAA LA WADAU WA MAJI ARUSHA
PICHANI: Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji , Profesa Kitila Mkumbo,Akizindua Jukwaa la wadau kuhusu usimamizi na utunzani wa maji katika Bonde la Pangani jijini Arusha juzi(Habari Picha na Pamela Mollel Arusha)
Na Pamela Mollel,Arusha
WIZARA ya Maji na Umwagiliaji, imeweka mkazo katika utunzaji wa maeneo ya vyanzo vya maji huku ikitaka wadau wa maji kushirikishwa kikamilifu katika mipango ya uanzishwaji wa viwanda.
Aidha imetaka sekta binafsi kushirikishwa katika usimamizi wa raslimali maji kwa kutoa elimu kwa wananchi kutovamia vyanzo vya maji huku ikiwataka waliovamia watoke. Akizindua Jukwaa la wadau kuhusu usimamizi na utunzani wa maji katika Bonde la Pangani jijini hapa jana, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Profesa Kitila Mkumbo, alisema, maji ni injini ya uchumi.
“Maji yanachangia ukuaji wa kila sekta, bila maji kwa mfano, hakuna viwanda, kilimo, ufugaji wala huduma zingine za kijamii. “Maji ni injini ya uchumi, lakini kwa bahati mbaya maji yamepungua wakati matumizi yake yakiongezeka kila siku,” alisema.
Akizungumzia hali ya maji nchini, alisema ina sura mbili, moja ni nchi yenye vyanzo vingi vya maji, wakati sura ya pili ni nchi inayokabiliwa na uhaba wa maji.
“Upungufu huu unatufanya kuona ulazima wa kutunza vyanzo vya maji vilivyopo kwa kushirikisha wadau na kutoa elimu kwa wananchi ili wasiendelee kuvamia maeneo ya vyanzo vya maji,” alisema na kuongeza, “waliovamia vyanzo hiyo watoke.”
Alisema kutokana na ongezeko la changamoto kuhusu usimamizi wa raslimali maji, anaamini sekta binafsi ambayo inategemea na kunufaika na matumizi ya maji ina jukumu kubwa la kufanya katika kutunza na kuhifadhi vyanzo vya maji.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa hilo, Mhandisi Mbogo Futakamba, alisema pamoja na vyanzo vingi vya maji vilivyopo nchini, lakini kuna changamoto katika matumizi kwa maendeleo ya kiuchumi.
Alisema kwa mfano, katika suala la uanzishaji wa miradi na viwanda ni lazima kupanga kwa pamoja wakianzia na suala la maji.
“Tukianza na maji tutapata viwanda, mifugo, kilimo na huduma za kijamii,” alisema.
Akizungumzia hali ya maji mkoani Arusha, Mhandisi wa Maji Mkoa, Joseph Makaidi, alisema, baadhi ya maeneo hali ya upatikanaji wa maji ni nzuri ikilinganishwa na maeneo mengine.
Alisema maeneo ya vijijini yanapata maji safi kwa asilimia 60.25 ingawa hayajatibiwa wakati maeneo ya mijini yanapata kwa asilimia 40.
Hata hivyo, alisema kuna tatizo la upatikanaji wa maji safi na kwa baadhi ya maeneo hususan, Arumeru kutokana na wingi wa madini ya fluoride katika maji.
Afisa Maji kutoka Bonde la Pangani, Mtoi Kanyawanah, alisema, inategemea na mvua inavyonyesha kwa mwaka.
Alisema kama kuna mvua nzuri kwa mwaka upatikanaji wa maji katika Bwawa la Nyumba ya Mungu na Hale na maeneo mengine unakuwa mzuri.
Kwa ujumla, “hali ya maji siyo nzuri wala siyo mbaya, na hii inategemeana na unyeshaji wa mvua.”
Pamoja na wadau wengine, uzinduzi wa jukwaa hilo ulishirikisha wawakilishi kutoka taasisi za International Water Stewardship Programme (IWaSP), Ukaid na GIZ.
Mwenyekiti wa Jukwaa Jukwaa la wadau kuhusu usimamizi na utunzani wa maji katika Bonde la Pangani Mhandisi Mbogo Futakamba, alisema pamoja na vyanzo vingi vya maji vilivyopo nchini, lakini kuna changamoto katika matumizi kwa maendeleo ya kiuchumi.
Mhandisi wa Maji Mkoa wa Arusha, Joseph Makaidi, alisema, baadhi ya maeneo hali ya upatikanaji wa maji ni nzuri ikilinganishwa na maeneo mengine.
Afisa Maji kutoka Bonde la Pangani, Mtoi Kanyawanah,akizungumza na vyombo vya habari
Baadhi ya washiriki wakiwa katika picha ya pamoja
MWISHO
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment