Thursday, October 19, 2017

CWT KOROGWE YAFURAHIA SERIKALI KULIPA MABILIONI YA WALIMU

PICHANI: Katibu wa CWT Mkoa wa Tanga Luya Ngonyani akizungumza jambo kwenye Mkutano Mkuu wa CWT Wilaya ya Korogwe uliofanyika mjini Korogwe. (Picha na Yusuph Mussa).

CHAMA cha Walimu Tanzania (CWT) kimeishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuwa sikivu baada ya kuahidi kulipa malikimbizo yasiyo ya mishahara sh. bilioni 48 na madeni ya mishahara ya walimu 12,899 ya sh. bilioni 13.3 kwa nchi nzima.

Hayo yalisemwa jana (19) na Mwenyekiti wa CWT Wilaya ya Korogwe David Nkingwa kwenye Mkutano Mkuu wa chama hicho Wilaya ya Korogwe, ambapo Mkuu wa Wilaya hiyo Mhandisi Robert Gabriel ndiyo alikuwa mgeni rasmi.

"Mgeni rasmi, tunaishukuru Serikali kwa kufanya majadiliano na viongozi wa CWT Makao Makuu Agosti 14, 2017, ambapo Serikali kupitia Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, ilikubali kuweka nyongeza ya mwaka kuanzia Septemba 2017, ambapo Rais Dkt. John Magufuli amekubali, na nyongeza itaanza kutolewa hivi karibuni.
"Malimbikizo ya madeni yasiyo ya mishahara sh. bilioni 48 nchi nzima yataanza kulipwa kwa walimu husika hivi karibuni. Pia malimbikizo ya madeni ya mishahara ya walimu 12,899 hadi kufikia Agosti 14, 2017 yalikuwa sh. bilioni 13,362,512,049 yalikuwa yamehakikiwa, na Serikali imekubali kuyalipa" alisema Nkingwa.

Nkingwa alisema Serikali itafanya urekebishaji wa mishahara kwa walimu wote waliopewa barua za kupanda madaraja. Walimu 80,000 walipandishwa madaraja na kupewa barua kwa mwaka 2015/16, lakini zoezi la urekebishaji mishahara lilisimamishwa kutokana na zoezi la kuondoa watumishi hewa na vyeti vya kughushi.

"Serikali iliahidi kuwa urekebishaji wa mishahara utafanyika baada ya kumalizana na waliokata rufaa ambao mwisho wake ilikuwa Septemba 30,2017, hivyo tutegemee mwishoni mwa Oktoba au Novemba, 2017 marekebisho hayo kufanyika. Upandishwaji wa madaraja kwa mwaka 2017/18, ambapo baada ya zoezi la kuhakiki vyeti na wafanyakazi hewa, Serikali imekubali kupandisha madaraja walimu 150,000" alisema Nkingwa.

Nkingwa alisema kwa Wilaya ya Korogwe, baada ya zoezi la uhakiki lililofanyika na kusimamiwa na Katibu wa CWT Mkoa wa Tanga Luya Ngonyani, madai ya walimu kwa jumla ni sh. milioni 504.3, ambapo mishahara ni sh. 248,307,883, uhamisho sh. 6,878,660 na masomo sh. 57,353,896.

"Matibabu sh.12,575,810, mazishi sh.211,000, likizo sh. 4,280,200, posho ya usumbufu sh. 27,210,160, wastaafu sh. 33,303,400 na madai mengine sh. 13,260" alisema Nkingwa.
 Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CWT Wilaya ya Korogwe wakimsikiliza Mwenyekiti wa chama hicho David Nkingwa wakati wa mkutano huo leo mjini Korogwe.

 Mwenyekiti wa CWT Wilaya ya Korogwe David Nkingwa akitoa taarifa mbele ya Mkutano Mkuu wa CWT Wilaya ya Korogwe uliofanyika leo Ukumbi wa St. Rock mjini Korogwe. Kushoto ni Katibu wa CWT Wilaya ya Korogwe Festo Mitimingi, wa tatu kutoka kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Mhandisi Robert Gabriel, wa tatu kutoka kulia ni Mwenyekiti wa CWT Mkoa wa Tanga Sufian Mussa na wa pili kulia ni Katibu wa CWT Mkoa wa Tanga Bi. Luya Ngonyani. (Picha na Yusuph Mussa).


No comments:

Post a Comment