Katibu Wa Halmashauri Kuu Ya Chama Cha Mapinduzi (NEC), Itikadi na Uenezi Ndg Humphrey Polepole akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Sekretarieti, Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam.
Waandishi wa habari wakimsikiliza kwa makini Katibu Wa Halmashauri Kuu Ya Chama Cha Mapinduzi (NEC), Itikadi na Uenezi Ndg Humphrey Polepole katika Ukumbi wa Sekretarieti, Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam.
Na Mathias Canal, Dar es salaam
Chama cha Mapinduzi kimesema kuwa
kipo tayari kuingia katika uchaguzi mdogo wa Ubunge Jimbo la Longido
Mkoani Arusha mara baada ya kutangazwa kuwa jimbo hilo lipo wazi
kutokana na maamuzi ya mahakama ya Rufaa iliyobainisha kuwa uchaguzi wa
mwaka 2015 haukuwa huru na haki hivyo kufuta matokeo ya uchaguzi huo.
CCM
imeeleza kuwa kulikuwa na matumizi yasiyostahili kutumika kujazwa
matokeo ya Ubunge, kwa kutumia fomu namba 21c za kujaza matokeo ya
Udiwani na kujaza matokeo ya Ubunge, badala ya kutumia fomu namba 21b
jambo lililopelekea kufungua kesi ya kupinga ushindi wa Ubunge katika
Jimbo hilo.
Kauli ya CCM imetolewa na Katibu Wa Halmashauri Kuu
Ya Chama Cha Mapinduzi (NEC), Itikadi na Uenezi Ndg Humphrey Polepole
wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Sekretarieti,
Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam.
Polepole
alisema kuwa vipo vyama vya siasa ambavyo kwa kawaida hulalamika kila
vinaposikia kushindwa na mahakama kwa madai kuwa hakuna haki lakini
vyama hivyo kila vinaposhinda vyenyewe husema mahakama imetenda haki.
Alisema
kuwa kazi ya mahakama ni kutumia sheria zilizopo na kuamua juu ya
malalamiko ya wananchi kwa kuhakikisha usawa mbele ya sheria kwa watu
wote unatendeka hivyo maamuzi yaliyotolewa juu ya kuwa wazi kwa Jimbo la
longido ni sehemu ya maamuzi huru na haki kwa mahakama ya Rufaa nchini.
Polepole
alitoa Rai kwa mahakama zote nchini kuendelea kufanya kazi yake vizuri
kwa uhuru na haki pasina kusikiliza kelele za watu wanaotaka mahakama
kutekeleza matakwa yao kinyume na sheria za nchi.
Kwa upande wake
aliyekuwa mgombea Ubunge wa Jimbo la Longido kupitia Chama Cha
Mapinduzi Dkt Steven Kiruswa akizungumza katika mkutano huo na waandishi
wa habari alisema kuwa pamoja na mapingamizi ya mara kwa mara katika
kipindi chote tangu rufaa ilipoanza kusikilizwa aliamua kuwa mtulivu kwa
kusubiri maamuzi yatakayotolewa na mahakama kama chombo huru nchini cha
maamuzi.
Alisema kuwa kwa mara ya nne mahakama ya Tanzania
imethibitisha kuwa inaongozwa kwa mujibu wa sheria na kujali haki ya
mwenye haki ili isipotee bure.
Alisema CCM ilifungua kesi
mwanzoni mwa mwezi Novemba 2015 ikiwa ni wiki mbili tangu kumalizika
uchaguzi mkuu uliofanyika Octoba 25, 2015 ambapo mahakama kuu ya Arusha
ilibaini kwamba uchaguzi haukuwa huru na haki na kufikia June 29, 2016
hukumu ikatolewa na ubunge kutenguliwa jambo ambalo liliwafanya Chadema
kukata rufaa zaidi ya mara tatu.
Dkt Kiruswa alisema kuwa
wananchi wa Longido wamenyanyasika katika kipindi cha miaka miwili
pasina kuwa na muwakilishi wa kuwasemea bungeni hivyo maamuzi ya
mahakama yataifanya Tume ya Uchaguzi kutangaza rasmi uchaguzi mdogo na
hatimaye muwakilishi kupatikana kwa kura za haki.
Aidha, Polepole
alisema kuwa Chama Cha Mapinduzi katika muktadha wa CCM mpya Tanzania
Mpya kinaendelea kusisitiza siasa safi na kutoa uongozi bora.
Alisema
siasa za kutumia lugha isiyofaa, na Siasa za aina yoyote zenye mtazamo
wa fitina hazina nafasi ndani ya Chama Cha Mapinduzi katika kipindi hiki
ambacho Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM
Mhe Dkt John Pombe Magufuli anaongoza kwani amedhamiria CCM kuwa chama
cha wananchi wote chenye mtazamo chanya katika uwajibikaji.
Alitoa
Rai kwa vyama vingine nchini kufanya siasa za weledi pasina kutumia
lugha za kuudhi dhidi ya serikali na wananchi wake huku akiahidi kuwa
chama chake hakiwezi kupoteza muda kujibu porojo za hila kwani kitakuwa
hakitendi haki katika kuisimamia ilani ya uchaguzi ya mwaka 2015-2020
kwa kuwaletea maendeleo endelevu wananchi.
Polepole alisema kuwa
CCM inaamini katika majibizano ya hoja kwani chama hicho kina deni kubwa
kwa wananchi la kuwaletea maendeleo hivyo viongozi wote wa chama na
wale wenye dhamana katika dola kuendelea kuishi misingi ya CCM Mpya ya
Uadilifu, Uaminifu, Uchapakazi, Vita dhidi ya Rushwa, Vita dhidi ya
ubadhilifu wa mali za chama na mali za Umma, Unyenyekevu na kusikiliza
watu.
MWISHO
Aliyekuwa mgombea Ubunge wa Jimbo la Longido kupitia Chama Cha Mapinduzi Dkt Steven Kiruswa akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Sekretarieti, Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam. Kushoto kwake ni Katibu Wa Halmashauri Kuu Ya Chama Cha Mapinduzi (NEC), Itikadi na Uenezi Ndg Humphrey Polepole
No comments:
Post a Comment