Thursday, August 17, 2017

MAANDALIZI YA IKUNGI ELIMU CUP 2017 YAPAMBA MOTO


Na Mathias Canal, Wazo Huru Blog

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu Jana Agosti 16, 2017 ametembelea na kukagua uwanja utakaotumika kwa ajili ya Mashindano ya ligi ya mpira wa miguu Wilayani Ikungi Mkoani Singida Maarufu kama “IKUNGI ELIMU CUP 2017”

Mhe Mtaturu akiwa ameongozana na Viongozi Mbalimbali katika Wilaya hiyo amezuru katika Uwanja wa shule ya Sekondari Ikungi ili kujionea Hatua za mwisho za maandalizi ya mashindano hayo.

Akizungumza na Mtandao wa www.wazo-huru.blogspot.com Mhe Mtaturu alisema kuwa mashindano hayo yataanza kurindima Siku ya Jumamosi Agosti 19 huku yakiwa na dhamira ya kuwafikia zaidi ya wananchi 5000 katika Wilaya hiyo.

Mashindano hayo yatakayofunguliwa na Mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe Dkt Rehema Nchimbi na kuzikutanisha timu mbalimbali kutoka Kata zote 28 na vijiji 101 katika Wilaya ya Ikungi huku yakiongozwa na kauli mbiu ya “ Changia, Boresha Elimu Ikungi”.

Mechi ya ufunguzi itakuwa ni kati ya timu ya Kata ya Ikungi na Timu ya Kata ya Puma ambapo kabla ya kufunguliwa kwa mashindano hayo kutakuwa na mchezo dhidi ya Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Singida waatakaovaana vikali na Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi.

Katika mchezo huo wa awali Timu ya Madiwani kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Ikungi itaongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji J. Mtaturu huku timu ya Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Singida ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhe Elias Tarimo.

Katika ufunguzi wa mashindano hayo kutakuwa na zoezi la Uzinduzi wa zoezi la ufyatuaji matofali ambapo kila Kata imetakiwa kufyatua matofali 10,000 ikiwa ni sehemu ya kuhimiza utatuzi wa Changamoto mbalimbali Wilayani Ikungi ikiwemo Upungufu wa nyumba za walimu, Vyumba vya madarasa, Ofisi za walimu, Maabara, Thamani mbalimbali, Matundu ya vyoo vya walimu na wanafunzi.
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu aliteuliwa kuwa mlezi wa mfuko wa Elimu kuhakikisha anahamasisha wananchi na wadau wachangie ili kufanikisha kuboresha miundombinu ya elimu katika wilaya ya Ikungi.

Mtaturu Alisema kuwa Uzinduzi wa ufyatuaji matofali umeanzishwa kwa ajili ya majukumu muhimu kusaidia sekta ya Elimu ikiwa ni pamoja na kuendeleza ujenzi wa maabara uliokwama toka mwaka 2009.

Mtaturu alisema kuwa katika ufunguzi wa mashindano hayo pia kutakuwa na zoezi la kukabidhi zawadi kwa shule ya sekondari Ikungi iliyofanya vizuri katika matokeo ya kidato cha sita na kupelekea kuongoza kikanda kwa wanafunzi 16 kupata Daraja la kwanza.

Kuanza kwa mashindano hayo ya “IKUNGI ELIMU CUP 2017” ni utekelezaji wa Wazo la kuanzisha Mfuko wa Elimu lilitokana na kikao cha wadau wa elimu kilichoitishwa na Mkuu huyo wa Wilaya mwezi Disemba, 2016 na kubaini changamoto zinazoikabili sekta ya elimu ikiwemo kushuka kwa ufaulu wa wanafunzi kuanzia elimu ya msingi mpaka Sekondari.










No comments:

Post a Comment