Na Jovin Mihambi, Mwanza
BAADHI ya wananchi waishio katika Mtaa wa Kuzenza, Kata ya Butimba wilayani Nyamagana katika hali isiyo ya kawaida wameonekana wakigombania nyama ya fisi ambayo iligongwa na gari katika maeneo ya Nganza Bodeni katika barabara itokayo Nyegezi Kona kuelekea Chuo cha Mtakatifu Augustini (SAUT) majira ya saa 12.00 alfajiri ya Julai, 2017 na kuleta tafrani kubwa miongoni mwa wakazi hao.
Shuhuda wa tukio hilo ambaye alijitambulisha kwa jina la Bw Laurent Mathayo, ambaye ni mwendesha bodaboda, alisema kuwa wakati akiongozana na gari hiyo ambayo hakutambua namba zake za usafiri, alishtukia ikigonga mnyama huyo na dereva wake hakusimama na kulikimbiza gazi kuelekea maeneo ya Chuo cha Mtakatifu Augustin (SAUT).
Alisema kuwa baada ya kuteremka katika pikipiki, alishtukia fisi huyo akigaragara pembeni mwa barabara hiyo na baadaye kukata roho na mda mchache baadhi ya waendesha bodaboda kutoka maeneo ya Nyegezi Kijiweni na Nganza ndipo walianza kuzingira mzoga huo na kuanza kuchuna ngozi yake, kumkata miguu pamoja na shingo na kuelekea katika maeneo yasiyojulikana.
Aidha, majira ya saa 2.00 asubuhi, gazeti hili lilifika eneo la tukio na kukuta baadhi ya wananchi katika mtaa wa Kuzenza (majina yanahifadhiwa) na wengine kutoka mitaa ya jirani ya Igubinya, Nyamarango na Sweya wakikata vipande vya nyama kila mtu sehemu ambayo alikuwa amekusudia kuwa ni muhimu kwake na wengine waliondoka na ngozi ya fisi huyo na kutokomea kusikojulikana.
Mkazi mmoja wa Mtaa wa Kuzenza ambaye alijitambulisha kwa jina la Mzee Shaban Yusufu (70) aliliambia gazeti hili kuwa hiyo ni mara ya pili fiki kugongwa katika eneo hilo na baadaye watu kufurika na kukata viuongo vyake na kudai kuwa wakati mwingine watu wanaofanya hivyo ni kutokana na imani za kishirikina na kusema kuwa tukio liliwahi kutokea mwaka 2005 katika eneo hilo.
"Wengine kutokana na imani zao, hudai kuwa kila kiungo cha fisi huweza kutibu maradhi mbali mbali ya binadamu na mkia wake ndiyo muhimu zaidi kutokana na wale wanaoruka kwa ungo kutokana na masuala ya ushirikina hutumia mkia huo kwa kuongoza chombo kikiwa hewani", alisema Mzee Yusufu.
Naye Msaidiza wa Mwenyekiti wa Mtaa wa Kuzenza Bw Mafuru Magambo, alisema kuwa kwa sasa kumekuwa na fisi wengi ambao hurandaranda nyakati za usiku na kuwataka wazazi kuchunga watoto wao hususani kutowatuma dukani wakati hiyo ili wasiweze kushambuliwa na fisi hao.
Naye Ofisa mmoja katika Ofisi ya Mwanasheria wa Serikali Kanda ya Mwanza ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini kwa vile siyo msemaji, alisema kuwa kukutwa na nyara za serikali ikiwa ni pamoja na ngozi ya fisi au viungo vyake, ni kifungo cha miaka mitatu jela au faini isiyopungua shilingi milioni 15 au vyote kwa pamoja.
No comments:
Post a Comment