Sunday, July 24, 2016

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

WAKATI wasanii wa kundi la ngoma za utamaduni la Utandawazi wanajipanga kutumbuiza, watu wengi waliokusanyika kwenye viwanja wa shule ya msingi Bukongo mjini Nansio walikuwa wanajiuliza mtoto Gozbert Bwele (8) aliyekuwa amekumbatia ngoma alikwenda kufanya nini pale.

Lakini mara tu ngoma zilipoanza kupigwa, uwanja mzima ukalipuka kwa furaha na haikushangaza wakati makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandez de la Vega, aliposhindwa kuvumilia na kutoka kwenda kucheza na mtoto huyo aliyeonyesha ufundi mkubwa katika upigaji wa ngoma.

Mama Maria Teresa, ambaye ni rais wa taasisi ya Mfuko wa kusaidia Wanawake Afrika, alijitoma uwanjani kucheza na kumtunza mtoto huyo anayesoma darasa la kwanza kwenye shule ya msingi Nansole katika halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza.





Makamu huyo wa rais mstaafu wa Hispania alizuru kisiwani Ukerewe akiwa ameongozana na ujumbe wake kwa lengo la kujionea kilimo cha viazi lishe na usindikaji wa mazao mbalimbali yatokanayo na viazi hivyo.

Kilimo hicho kinafanywa na akinamama 25 chini ya Mradi wa Green Voices unaofadhiliwa na taasisi ya Mfuko wa kusaidia Wanawake Afrika, ambao kwa hapa nchini umewawezesha wanawake wa Tanzania kubuni miradi endelevu inayoendana na utunzaji wa mazingira pamoja na kupambana na mabadiliko ya tabianchi.



No comments:

Post a Comment