Monday, June 13, 2016

LEONCE MULENDA: KIJANA MSOMI MWENYE NDOTO YA KUWA KIONGOZI WA JUU TANZANIA

 * 'Alikula sahani moja' na vigogo kuwania Urais na Uspika wa Bunge 2015
* Ni msomi wa Shahada ya uzamivu (PhD) katika masuala ya usimamizi wa Biashara
* Asema Dk. Magufuli atarejesha nchi katika misingi ya Mwalimu Nyerere

NA BASHIR NKOROMO
Baada ya Uchaguzi Mkuu uliofayika mwezi Oktoba, 2015, na kuiacha Tanzania ikiwa na Rais wa awamu ya tano, ambaye ni Rais Dk. John Pombe Magufuli, yapo mambo mengi yamebaki katika kumbukumbu za Watanzania walio wengi.

Kwa upande wa mchakato ndani ya CCM wa kuwapata wagombea kwenye nafasi hizo, yapo mengi ya kukumbukwa, lakini mojawapo ni majina ya waliokuwa mstari wa mbele katika vinyang'anyiro katika nafasi mbalimbali vilivyokuwa katika Uchaguzi huo Mkuu, ikiwemo kinyang'anyiro cha Urais, Makamu wa Rais, Uspika, Wabunge/ Wawakilishi na madiwani.

Walioshiriki katika kinyang'anyiro hicho wamebaki katika kumbukumbu za vichwa vya Watanzania kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo namna walivyokuwa wakionyesha ushiriki wao katika kuomba nafasi wanazoziomba kugombea kwa tiketi ya CCM, baadhi yao wakiwa vigogo na wengine ikiwa ni mara yao ya kwanza kuwania uongozi wa juu nchini.

Bila Shaka, Kijana Leonce Mulenda ni miongoni mwa wanachama wa CCM wanaokumbukwa  kutokana na umahiri alioonyesha wakati akishiriki katika kinyang'anyiro hicho.

Kwa waliofuatilia kwa karibu kinyang'anyiro cha kuwania nafasi ya urais na Uspika wa Bunge, ndani ya CCM watakubali kwamba  Mulenda mwenye umri wa miaka 44, ni kijana anayeonyesha ari, utashi na hamu kubwa ya kutaka kuwatumikia Watanzania katika kulijenga Taifa.

Katika harakati zake za kuonyesha ari, utashi na hamu ya kutaka kuwatumikia Watanzania, wakati wa vuguvugu hilo la Uchaguzi Mkuu uliomalizika mwaka jana wa 2015, Mulenda ni miongoni mwa Wanachama wa CCM, walioingia kwa kasi kubwa  katika kinyang'anyiro cha kuomba kuteuliwa kugombea Urais kwa tiketi ya CCM.


Mulenda ambaye alizaliwa Januari 25, 1972, Biharamulo mkoani Kagera, katika kudhihirisha kuwa hakuwa akifanya mzaha, baada ya kuchukua fomu ya kuwania kuteuliwa kugombea urais kwa tiketi ya CCM, aliweza kutembea katika mikoa 15 ikiwemo mitatu ya Zanzibar, na kupata wadhamini 450 waliotakiwa kwa mujibu wa utaratibu.

Wakati wapo baadhi ya waliochukua fomu za kuomba kuteuliwa kuwania nafasi hiyo ya Urais, walishindwa kujerejesha fomu zao, Mulenda aliweza kuwasilisha fomu zake Juni 25, 2015, kwa Katibu wa NEC, Oganaizesheni Dk. Mohammed Seif Khatib ambaye alipangwa kupokea fomu za wagombea wote kwa niaba ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana.

Baadaye katika mchakato wa kumpata mgombea Urais, Mulenda alibaki miongoni mwa makumi ya waliokosa kuteuliwa, katika hatua za awali wakiwemo, vigogo wengi kama aliyekuwa Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Bilali, Mawaziri Wakuu wastaafu Frederick Sumaye na Edward Lowassa.

Japo wengine waliamua kuisusa CCM na kuamua kuhamia vyama vya upinzani akiwemo Lowassa na Sumaye, kada huyo wa CCM, Mulenda ni miongoni mwa wanachama waliokosa kuteuliwa lakini wakaridhika kwa sababu walifahamu kuwa katika mchakato wa uchaguzi wagombea wakiwa wengi na nafasi ni moja lazima wawepo wanaokosa.

Kadhalika wanachama hao wa CCM ambao hawakuteteleka akiwemo Mulenda, walitambua kwamba, ikiwa lengo lao ni kuongoza Watanzania, si lazima waongoze wakiwa tu katika nafasi ya Urais wanaweza kuongoza wakiwa katika eneo lolote la uongozi na pia ikiwa kiu yao ni urais basi uchaguzi wa 2015 siyo wa mwisho ikiwa kiyama hakitatokea hivi karibuni hivyo wakati ukijiri tena watagombea.

Baada ya kivumbi cha mchakato wa kuomba kuteuliwa kuwania urais kwa tiketi ya CCM kupita, kiliingia kingine cha kuwania nafasi ya Uspika wa Bunge, ambapo katika kinyang'anyiro hiki nako walijitosa wagombea wengi tena vigogo ambao ni mahiri akiwemo Spika wa zamani Samweli Sitta.

Kwa kufahamu kwamba demokrasia inamruhusu, Mulenda naye aliingia pia kuwania nafasi hiyo ya kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo alichukua fomu Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Mtaa wa Lumumba jijini Dar es Salaam, na baadaye kuirejesha ikiwa imekamilika kujazwa kwa usahihi.

Hata hivyo katika kinyang'anyiro hicho pia hakupita, na siyo yeye tu, walikosa wengi kwa kuwa walioomba walikuwa lukuki na kama ilivyokuwa kwa urais, nafasi ya Uspika wa Bunge nayo ilikuwa moja, hivyo ilikuwa lazima wawepo watakaokosa miongoni mwa wagombea.

Baada ya michakato hiyo sasa Mulenda anaendelea na shughuli zake akiendelea kuamini kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) ndicho chama pekee nchini kitakachoweza kuwakomboa Watanzania kuelekea maisha bora.

"Unajua wapo watu wanaodhani kuwa kipo Chama kinachoweza kuwa mbadala wa CCM katika kuwaletea maendeleo wananchi, fikra hizo ni potofu kabisa, CCM bado ndicho chama pekee, imara na chenye sera bora zinazotekelezeka tofauti na vyama vingine", alisema Mulenda ambaye ana kadi ya CCM yenye namba Ab 1353192.

Anasema, anaamini CCM ndicho chama kinachofaa kuongoza Watanzania kwa sababu ya uwezo wake ambao umejengwa chini ya misingi imara iliyowekwa na muasisi wake, Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Nyerere tangu enzi za chama cha Tanganyika African National Union (TANU) ambacho CCM inaendeleza misingi yake.

"Kwa kuwa misingi iliyowekwa na Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere na Hayati Abeid Aman Karume kwa upande wa Zanzibar, bado ni imara hadi sasa, CCM haiwezi kutetereka hasa ikizingatiwa kwamba katika misingi hiyo iliyowekwa na Baba wa Taifa ni yenye mlengo endelevu wa kujali hali za wanyonge", alisema Mulenda.

Anasema, kitu ambacho huteteresha na baadhi ya watu kudhani CCM si chama cha wanyonge, ni kutokana na baadhi ya viongozi kusahau au kuipuuza misingi hiyo iliyowekwa na Baba wa Taifa, na hivyo kuanza kujiwekea misingi bandia kwa lengo la kujinufaisha wao binafsi.

"Lakini sasa, baada ya Tanzania kumpata Rais Dk. John Magufuli,  hali inaelekea kubadilika na huenda ikaimarika kabisa kutokana na Rais huyu anavyojaribu kuiweka Nchi katika misingi ile iliyoasisiwa na Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere na Hayati Karume", alisema Mulenda.

Licha ya kupenda siasa, Mulenda ni msomi amabaye  kwa sasa anaendelea na masomo ya Shahada ya uzamivu (udaktari) katika masuala ya Usimamizi wa Biashara (PhD-Bus.Mgt. (on studies), mada anayotafiti katika masomo yake hayo ni "Effectiveness of Forecasting value chain on improving production costs of oil and gas through extractive induestries in Tanzania, na utafiti huo ataufanyia  katika Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC).

Wakati akiendelea na masomo hayo ya PhD, tayari alikwishafuzu Shahada ya Uzamivu ya Sayansi ya Uhasibu na Fedha (MSc. A&F) aliyopata mwaka 2014, katika Chuo Kikuu Cha Mzumbe Kampasi ya Dar es Salaam, akiwa  tayari  amemaliza Stashahada ya Uzamili katika fani ya Usimamizi wa Fedha (PGDFM) katika Chuo cha Uhasibu kilichopo Njiro mkoani Arusha, mwaka 2006.

Kabla ya kufikia kiwango hicho cha elimu, Mulenda alikuwa pia ameshahitimu Stashahada ya Juu  katika chuo Nyegezi Social Training Institute (NSTI) ambacho sasa ni Chuo Kikuu cha St. Augustine kilichopo Mwanza, mwaka 1998.

Mulenda kwa sasa ni mtumishi wa umma katika Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali akiwa katika cheo cha Mkaguzi wa Hesabu daraja la kwanza, na pia ni mwanzilishi na Mwenyekiti wa Asasi isiyo ya Serikali (NGo) ambayo inashughulikia masuala ya Kijamii katika kukuza uchumi  na kupunguza umasikini (Economic Growth and Social Welfare Foundation Gwrowth and Social Welfare-EGOSF), yenye usajili namba ooNGO/ooooo7736.

No comments:

Post a Comment