Friday, May 06, 2016

WABUNGE WANAWAKE WA UPINZANI WASUSIA BUNGE, WAPINGA KUITWA 'BABY'

Mtafaruku mpya umetokea kwa mara nyingine tena Bungeni ambapo wabunge wanawake kutoka vyama vya upinzani kutolewa bungeni kutokana na kupinga kudhalilishwa ambapo Wabunge hao walisimama mara baada ya kipindi cha maswali na majibu leo asubuhi kuomba mwongozo wa spika kuhusiana na matusi yaliyotolewa jana na Mbunge wa Ulanga Mashariki,Goodlack Mlinga (CCM),ambaye alidai ndani ya vyama hivyo ili uteuliwe katika nafasi ya viti maalum lazima uitwe ‘baby’.
Mlinga alikwenda mbali zaidi na kudai kwamba ndani ya vyama vya upinzani wabunge wanafanya mapenzi ya jinsia moja jambo lililozua sintofahamu baada ya wabunge wa upinzani kusimama wakidai wamedhalilishwa .
Dkt. Tulia alimpa nafasi ya kutoa mwongozo Mbunge wa Viti Maalum,Sophia Mwakagenda,(Chadema) ambaye aliomba mwongozo kuhusiana na kauli ya Mlinga akidai kwamba hawezi kuvumilia udhalilishwaji huo na kwamba ameamua kujitoa katika Chama Cha Wabunge Wanawake,(PWTG) ambacho moja ya majukumu yake ni kutetea haki za wanawake lakini hakijaonyesha kutetea ushalilishaji huo na kwamba wabunge wengine wanawake kutoa CCM walikuwa wanapiga makofi kushangilia udhalilishaji huo.
“Mheshimiwa Naibu Spika nimesimama kuomba mwongozo kwa kutumia kanuni ya 68 7 kutokana na sign tuliyosaini Maputo protocol,sitaki kuamini kwamba kila mwanamke anapitia mchakato wa uzinifu ili wapate uongozi,mimi kama mama na mwanaharakati,mfumo dume uliojikita kwa wanaume na wanasiasa,nataka unipe muongozo kama hii ni sahihi?”alihoji Sophia na kuongeza kuwa
’’Lakini tuna vyama vyetu vya kibunge kama PWTG leo hii mimi kama mwanachama natangaza kujivua kwasababu lengo la chama ni kutetea haki za wanawake wanaponyanyaswa lakini wanawake wenzetu walioko katika chama hicho wanaunga mkonona kushangilia udhalilishaji usiokuwa na vidhibiti,nataka suala hilo likome hata huko nje wanaofikiria kila mwanamke ni mdhinifu’’
Naibu Spika wa Bunge,Dkt. Tulia Ackson,alitoa ufafanuzi kuhusiana na mwongozo huo akisema ”Wabunge naombeni mtulie,Mheshimiwa Esther Bulaya,Tafadhalia,Esther Bulaya tafadhali,juzi nilitolea maelezo na kutolea ufafanuzi jambo hili kwamba pande zote hapa ndani huwa zinatoleana maneno yasiyofaa lakini nilisema maneno yale yafutwe yasiingie kwenye hansad,hivyo mtulie tuendelee,’’alisema
Hata hivyo kelele za kuomba mwongozo kwa wabunge hao ziliendelea lakini Dkt. Tulia hakusikiliza aliwaambia wakae na kuendelea kutangaza wageni waliokuwa wametembelea Bunge na aliwataja kwa majina wabunge waliokuwa wamesimama na kuwataka wakae ratiba ikaendelea.
Baada ya kumaliza kutambua wageni walioko bungeni wabunge hao walisimama kwa mara nyingine wakiomba mwongozo kuhusiana na jambo hilo lakini hakuwasikiliza aliendelea na ratiba ya kumtaka Waziri wa Viwanda,Biashara na Uwekezaji kusoma bajeti yake.
Jambo hilo halikukubalika na wabunge wanawake kutoka upinzani hivyo walisimama muda wote wakiongea kuomba mwongozo kwa madai kwamba kanuni za bunge zinaruhusu na hawataki kuburuzwa jambo lililozua kutoelewana ndani ya ukumbi kutokana na kelele.
Mbunge wa Kawe,Halima Mdee,alisikika akisema”Msituburuze usitumie kiti vibaya tuna haki kwa mujibu wa sheria,tunaomba kupewa nafasi ya mwongozo hatuwezi kuvumilia udhalilishaji huu”Dkt. Tulia alijibu “Waheshimiwa kaeni chini,waheshimiwa mliosimama kaeni chini,nimesema kaeni chini,mheshimiwa Upendo Peneza kaa chini ,’’ wabunge hao waliendelea kusimama huku wakitoa maneno lakini maiki zao zilikuwa zimezimwa hivyo hayakuwa yanasikika vizuri.
“Waheshimiwa wabunge mliosimama naomba mtoke nje,waheshimiwa wabunge mliosimama naomba mtoke nje,waheshimiwa wabunge tokeni nje,sagent naomba muwatoe nje wabunge waliosimama,wabunge waliosimama watoeni nje,sajenti watoeni nje wabunge wabunge waliosimama,’’alisema Dkt. Tulia
Wabunge hao wanawake wote kutoka upinzani walitolewa nje huku wakiwa wanazungumza maneno mengi ambayo yalikuwa hayasikiki kutokana na maiki kutowashwa lakini walivyotoka Mbunge wa Iringa Mjini,Mchungaji Peter Msigwa,aliendelea kuomba mwongozo lakini Dkt. Tulia alimkatalia jambo ambalo lilimfanya ajibu kwamba anawaburuza na haikubaliki na baada ya hapo naye alitoka nje hakuendelea kukaa katika kikao hicho.
Akizungumza kwa niaba ya wabunge hao,Mdee amesema spika alikuwa anawaburuza kwani kukataa kutoa mwongozo uliotokea juzi ni kwenda kinyume na katiba.
“Siku hizi Wanajificha wanaogopa wakiwa live tutawapiga uovu wao,ufisadi wao hivyo juzi walikuwa na kikao chao cha chama nadhani hayo ndiyo waliyokubaliana huko ili wajifiche na kuanza kututukana hatuwezi kukubali kudhalilishwa na upuuzi huu uendelee,hatutaki matusi’’anasema Mdee
Amesema kuwa wabunge wote wanawake wa Ukawa wamejitoa rasmi katika chama cha PWTG na kwamba watapeleka barua kwa Mwenyekiti wa Chama hicho,Magreth Sitta,kilichobaki kitakuwa chama cha wabunge wanawake wa CCM.
Anaongeza kuwa watakaa kama kambi ya Ukawa kuangalia utaratibu wa kuanzisha chama kingine,watapeleka kwa spika na viongozi wote wa bunge barua kwasababu chama hicho kipo kikanuni na watu wanatumia chama hicho kwenda katika vikao na wanapata fedha wakati chama hicho hakitusaidii.
Aidha amesema kuwa watapeleka nakala ya barua hiyo pia katika taasisi zote zinazowafadhili kuwajulisha kwamba wamejitoa na chama hicho ni cha wabunge wa CCM pekee ili wasiendelee kujikombea fedha wakati hakifanyi kazi ambazo zinatakiwa kufanyika.



No comments:

Post a Comment