Thursday, March 03, 2016

SERIKALI KUJENGA MACHINJIO YA KISASA VINGUNGUTI

Na MAELEZO
Serikali imejipanga kujenga machinjio ya kisasa katika eneo la Vingunguti Jijini Dar es Salaam ili kuondoa changamoto zilizopo machinjioni hapo ikiwa ni pamoja na kulinda afya za wachinjaji na walaji wa nyama.

Akiongelea mipango hiyo kwa njia ya simu Msemaji wa Manispaa ya Ilala Bi.Tabu Shahibu amesema Halmashauri iko katika mchakato wa kutangaza zabuni kwa makampuni yatakayoweza kujenga machinjio hayo kwa kiwango kinachotakiwa.

“Tupo katika harakati za kutafuta mkandarasi wa kujenga machinjio na hivi karibuni tutatangaza zabuni kwa ajili ya ujenzi huo”

“ Napenda kuwahakikishia kwamba tutafanya jitihada zote za kumpata mkandarasi mapema ili tuanze mapema ujenzi huu wa machinjio mapya na kuondokana na changamoto zinazokabili machinjio yaliyopo”Alisema Bi Tabu.

Aidha, Bi Tabu Shaibu amesema kuwa kabla ya kujenga machinjio mapya wanaendelea na ujenzi wa mabanda ya machinjio, njia za kushushia ng’ombe ,bucha na kupanua eneo la machinjio na wameshapima na kufanya tathimini ya gharama ambazo zitatumika katika marekebisho hayo.

Mpango huu umekuja mara baada ya ya agizo la mawaziri, akiwemo Waziri wa Kilimo,Mifugo na Uvuvi Mhe. Mwigulu Nchemba, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Hamis Kigwangalla na Waziri wa Nchi ofisi ya Raisi TAMISEMI MHE. George Simbachawene walipotembelea machinjio ya Vingunguti Januari 2 mwaka huu.

Machinjio ya Vingunguti yalianza kutumika tangu miaka ya 1950 ikiwa inahudumia idadi ya watumiaji wa mazao ya wanyama waliokuwa kwa wakati ule. Machinjio hayondio bado yanatumika hadi sasa wakati idadi ya watumiaji wa mazao ya nyama wameongezeka hivyo kukumbana na changamoto mbalimbali. Ili kukabiliana na changamoto hiyo Serikali imepanga kuyarekebisha yaliyopo na kujenga mapya na ya kisasa.

No comments:

Post a Comment