Thursday, March 17, 2016

SERIKALI KUANZISHA WAKALA WA USIMAMIZI WA MAAFA NCHINI











Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu,Sera na Uratibu Dkt Hamis Mwinyimvua akizungumza na wajumbe wa kamati ya maafa ya taifa(TANDTRADE)( Hawapo pichani) wakati wa kikao cha kamati hiyo kilichofanyika leo Jijini Dar es Salaam.

Na MAELEZO
Serikali imekusudia kuanzisha Wakala wa Usimamizi wa Maafa Tanzania chini ya Sheria ya mwaka 2004 ambao utakuwa na jukumu la kupambana na maafa yatakayojitokeza kwa kuratibu na kuwezesha waathirika wa maafa kupata misaada ya mahitaji muhimu kwa haraka.

Akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Maafa ya Taifa(TANDTRADE) Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu,Sera na Uratibu Dkt Hamis Mwinyimvua amesema Serikali imedhamiria kuanzisha Wakala wa Usimamizi wa Maafa ili kuweka utaratibu mzuri ambao utasaidia kushughulikia kwa umakini maafa yatakayokuwa yakijitokeza katika sehemu mbalimbali nchini.

“ Ipo Sheria ya Wakala wa Usimamizi wa Maafa basi ni jambo jema kuwepo kwa Wakala ili kuweza kuratibu vizuru shughuli za kupambana na maafa yanayotukumba”

“Tumekutana leo hapa katika kikao cha kawaida cha kupata taarifa juu ya maafa yanayotokea nchini na tutajadili na kutoa madhimio ambayo yatatoa majibu ya nini kifanyike katika kutatua changamoto zinazojitokeza wakati wa kupambana na maafa” Alisema Dkt Mwinyimvua.

Kamati ya Maafa ya Taifa iko chini ya mwenyekiti ambaye ni Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu,Sera na Uratibu ikiwa na wajumbe kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa, Wizara ya Afya,Ustawi wa Jamii,Watoto na Wazee, Jeshi la Zima Moto,Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano,Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo, Taasisi na Idara za Serikali zinazohusika na maafa.


No comments:

Post a Comment