Wednesday, March 02, 2016

MWANDISHI WA SIBUKA TELEVISION APIGWA DODOMA

Na Mwandishi Wetu, Mpwapwa.
MWANDISHI wa habari wa kituo cha Televisheni ya Sibuka Barnabas Kisengi amejikuta katika wakati mgumu mara baada ya kupigwa na kujeruhiwa na mwenyekiti wa kijiji cha Mtamba kata ya Rudi Wilaya ya Mpwapwa Mkoani Dodoma Moris Mapai na akiambatana na watu waliodaiwa kuwa ni wafuasi wake.

Tukio hilo limetokea jana katika kijiji hicho wakati mwandishi huyo alipokuwa ameambatana na waandishi wengine akiwemo mwandishi wa gazeti hili na mwandishi wa Azam TV walipokuwa kwenye majukumu yao ya kila siku.

Mwandishi huyo alisema kuwa tukio hilo limetokea jana majira ya asubuhi wakati akielekea nyumbani kwa mwenyekiti wa kijiji hicho anayetuhumiwa na wananchi kwa tuhuma mbalimbali ikiwemo kutowasomea mapato na matumizi pamoja na kutoitisha mikutano ya hadhara.

"Leo asubuhi(jana asubuhi) tulikuwa kwenye majuku yetu ya kila siku tukafika kijiji cha Mtamba tukawaona wananchi wa kijiji hiki wakiwa wamebeba mabango yenye jumbe mbalimbali pamoja na matofali wakielekea kwenye ofisi ya mwenyekiti wa kijiji wakidai kuwa wanaenda kuifunga ofisi hiyo.

"Baada ya hapo kama kawaida yetu tukafika eneo la tukio tukashuhudia wananchi wakijenga na matofali kwenye mlango wa ofisi hiyo ambapo zoezi hilo lilipoisha tukaenda kwa mwenyekiti wa kijiji hicho ambaye anatuhumiwa na wananchi wake ili kupata ukweli zaidi kuhusiana na tuhuma hizo"alisema Barnaba.

Aidha alisema kuwa baada ya wananchi kufunga ofisi hiyo walienda kukamilisha stori kwa mwenyekiti huyo kuhusu tuhuma zinazomkabili.

"Tulipofika nyumbani kwake tukashudia mwenyekitu huyo pamoja na wafuasi wake kadhaa wakiwa wamemteka afisa mtendaji kwa kata hiyo Gidion Ngosi aliyekuwa ametekwa na mwenyekiti wa kijiji hicho na kikosi chake kwa madai kwamba kwanini amefika katika ofisi hiyo ambako wananchi walikuwa wakifunga ofisi yake.

“Tulifika tukasalimia tulishangaa mwenyekiti huyo akisimama na kuanza kunipiga kibao huku akifuatiwa na wafuasi wake ambapo mmoja alichukua mnyoro wa baiskeli na wengine kuni na kuanza kunipiga navyo huku waandishi wenzangu wakifanikiwa kutimua mbilo na kutokomea kusikojulikana"alisema Barnaba.

Hata hivyo alisema kuwa baada ya hapo alifanikiwa kukimbia huku akiomba msaada kwa wananchi.

Hata hivyo alisema kuwa alifanikiwa kutoa taarifa kwa Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mohammed Utari na Kamanda wa polisi Mkoa wa Dodoma David Misime kuhusiana na tukio hilo.

Kwa upande wake mwandishi wa habari wa Azam TV Alen Silivery alisema kuwa anashangazwa na kitendo kilichofanywa na mwenyekiti huyo ambapo inaonekana kazi yake ya uenyekiti imemshinda.

“Kwa tukio hili la mwenyekiti kumpiga mwandishi inaonekana amechoka na kazi yake hivyo kuamua kuwa bondia”alisema Silvery.


No comments:

Post a Comment