Bwana Toshio Nagase ameyaeleza hayo akisema kuwa ni muendelezo wa ushirikiano wa Tanzania na Japan kama ilivyo kwenye sekta nyingine kama vile ya ujenzi na uchukuzi. Nchi yake iko tayari kuwekeza Tanzania kwa kushirikiana kwa pamoja kuendeleza Sekta ya Mawsiliano na TEHAMA nchini kupitia ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na Japan; au kampuni na sekta binafsi za Tanzania na Japan.
Bwana Nagase alisema kuwa Tanzania imepiga hatua katika matumizi ya simu za mkononi na huduma za mawasiliano ikiwemo huduma za kutuma na kupokea pesa kupitia kampuni za simu za mkononi. Hivyo nchi yake ya Japan iko tayari kuendeleza hilo kwa kuwawezesha watanzania kupata huduma nyingine kama vile bima ya afya kwa kupitia simu ya mkononi. “Sisi nyumbani mwananchi akipiga simu anapatiwa pointi ambazo zinamuwezesha kugharamia huduma ya bima ya afya. Jambo hili ni muhimu kwa wananchi wa Tanzania kupata huduma mbalimbali kupitia simu za mkononi” alisema Bwana Nagase.
Prof. Faustin Kamuzora alisema kuwa Tanzania imekuwa ni nchi ya kuigwa duniani na kupigiwa mfano kwa kuwawezesha wananchi kupata huduma ya kutuma na kupokea pesa kupitia simu za mkononi na kufanya malipo mbalimbali. Prof. Kamuzora aliongeza kuwa, “sisi kama Serikali tunawakaribisha wenzetu wa Japan kuja Tanzania kushirikiana nasi kuendeleza Sekta ya Mawasiliano na kuwekeza nchini kwetu ili wananchi wetu wanufaike na maendeleo ya Sekta hii kama ambavyo wenzetu wamepiga hatua kwa kuwa na kampuni za vifaa vya TEHAMA kama vile kampuni ya Sony”.
Kwa upande kwa Sekta ya Mawasiliano Prof. Kamuzora alisema kuwa Wizara iko tayari kuanzisha viwanda vya TEHAMA vya kutengeneza bidhaa na vifaa vya TEHAMA hapa nchini kwa ajili ya wananchi na kubuni programu mbalimbali za kompyuta ambazo zitarahisha na kutatua changamoto za wananchi kuendana na mazingira yetu ya Tanzania. Prof. Kamuzora aliongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ni Serikali inayotoa kipaumbele kwenye masuala ya ujenzi na uendeshaji wa viwanda hapa nchini hivyo Sekta ya Mawasiliano ina nchango mkubwa wa kuiwezesha sekta binafsi na wawekezaji kuendeleza Sekta ya Mawasiliano hivyo kuongeza fursa ya ajira kwa vijana.
Bwana Nagase amesema kuwa JICA iko tayari kushirikiana na Wizara kuwakutanisha wafanyabiashara; wawekezaji; kampuni; sekta binafsi na wadau mbalimbali wa Sekta ya Mawasiliano wa Tanzania na Japan ili kubadilishana uzoefu na kuainisha fursa na maeneo ya kushirikiana kwa lengo la kuendeleza sekta hiyo na ushirikiano wa nchi hizo mbili kwenye Nyanja ya TEHAMA.
Aidha, Prof. Kamuzora na mgeni wake Bwana Nagase wamekubaliana kuainisha maeneo ya kipaumbele ambayo yatafanyiwa kazi kwa pamoja ili kufanikisha uwekezaji kwenye maeneo hayo ikiwa ni pamoja na kuwapatia mafunzo na ujuzi watanzania; kuendeleza vijana wenye kampuni zinazohusika na masuala ya ubunifu kwenye TEHAMA na kuwekeza pia.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
No comments:
Post a Comment