Na Raymond Mushumbusi-MAELEZO)
Shillingi Billioni 60 zinategemea kutumika kufufua kiwanda ya matairi cha General Tyres kilichopo Jijini Arusha ambacho kimesharudi mikononi mwa Serikali, na fedha hizo zitatumila kurekebisha mitambo ya umeme ya kiwanda hicho na kupata mitambo mipya itakayoendana na teknolojia ya utengenezaji wa matairi duniani.
Akijibu swali la Mhe. Joshua Nassari Mbunge wa Arumeru Mashariki (CHADEMA) lililouliza ni lini serikali itafufua kiwanda cha matairi cha General Tyres kilichopo Jijini Arusha kwani ni tegemeo kwa ajira kwa wananchi wa Jijini la Arusha,Waziri wa Viwanda,Biashara na Uwekezaji Mhe.Charles John Mwijage amesema kiwanda hicho kimesharudi mikononi mwa Serikali na wako mbioni kukifufua ili kianze kufanya kazi ya kuzalisha matairi nchini.
“ Tumeanzisha viwanda nchi ili kuzalisha bidhaa na kutoa ajira kwa watanzania na sio kuwatesa wananchi kwa kukosa ajira au kuagiza bidhaa ambazo tunaweza kuzalisha hapa hapa nchini, hivyo basi Serikali kupitia Wizara yangu tutatenga fedha kwa ajili ya kufufua kiwanda hiki ili kianze kufanya kazi mara moja”
“ Sio tu tutafufua kiwanda cha General Tyres pekee bali tunafatilia viwanda vyote ambavyo vimekiuka sheria na kanuni kwa kutoviendeleza viwanda hivyo ili kuvirudisha mikononi mwa Serikali au kuwatafuta wawekezaji wengine watakaoweza kuviendesha viwanda hivyo” Alisema Mhe. Mwijage.
Aidha Mhe. Charles John Mwijage amesema ni kweli makampuni mengi yaliyobinafsishwa hayakufanya vizuri katika uendeshaji wake ukiacha mifano ya makampuni machache yanayofanya vizuri yakiwemo Tanzania Breweries Limited (TBL),Morogoro Polyester 21st Century na Tanzania Cigarette Company Limited (TCC), hivyo Wizara yangu ikishirikiana na Msajili wa Hazina juu ya Viwanda ilifanya tathmini iliyoonesha kuwa mashirika mengi yaliyobinafsishwa hawakutekeleza mikataba ya mauziano kikamilifu.
Ameongeza kuwa lengo ni kuhakikisha makampuni yote haya yanazalisha kwa tija ili tupate bidhaa,kodi ya Serikali na ajira kwa wananchi wa Tanzania ili kutimiza adhma ya Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.John Pombe Joseph Magufuli ya kuwa na Tanzania yenye viwanda kwa maendeleo ya taifa.
Serikali kupitia Wizara yetu inaboresha mazingira ya uwekezaji hali itakayowajengea imani kwa wawekezaji na kupelekea kupanua zaidi shughuli zao za kibiashara na pia kuendeleza mpango wa Viwanda vidogo na vya kati unaoshirikisha SIDO na Halmashauri za Wilaya na Mikoa ili kuanzisha Viwanda vya Mkoa vya kuongeza thamani ya bidhaa za Kilimo,Uvuvi na ufugaji kupitia njia hii ajira nyingi zitaongezeka na kupunguza tatizo la ajira nchini.
No comments:
Post a Comment