Saturday, January 23, 2016

WAZIRI KITWANGA: KAMATAMATA KWA RAIA WA KIGENI, HAITAGUSA WENYE VIBALI HALALI (PICHA)


Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick akimpongeza Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga (kushoto), kwa kutoa hotuba nzuri iliyowafafanulia wachina waishio nchini kuwa Serikali ya Tanzania inawajali na inatambua umuhimu wa ushirikiano wao uliodumu kwa kipindi cha miaka mingi, hivyo raia yeyote wa kigeni anatakiwa afuate taratibu za kuishi Tanzania, na operesheni inayoendelea ya kuwakamata raia wa kigeni nchini, kamwe haitagusa wenye vibali halali. Wachina waishio nchini jana walifanya sherehe ya kuukaribisha mwaka mpya iliyofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip na kuhudhuriwa na mamia ya wachina hao. Kulia ni Kaimu Balozi wa China nchini, Zhang Biao.


Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Charles Kitwanga amesema zoezi linaloendelea sasa la kukamata raia wa kigeni wanaoishi na kufanya kazi hapa nchini bila vibali halitawagusa wageni wenye vibali halali.

Mheshimiwa Kitwanga ameyasema haya mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na jumuiya ya raia toka nchini China wakati wa sherehe zilizoandaliwa na raia hao katika Hoteli ya Golden Tulip jijini Dar es Salaam.

Katika sherehe hizo ambazo ziliandaliwa mahsusi kuukaribisha mwaka Mpya wa Kichina, Mheshimiwa Kitwanga alisema uhusiano wa Tanzania na China ulianzishwa na marehemu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Kiongozi wa China, marehemu Mao Zedong zaidi ya miaka hamsini iliyopita.

Amesema uhusiano huo umeendelea kuimarishwa hadi katika nyanja za kiuchumi ambapo hadi sasa kuna zaidi ya Kampuni 500 za Kichina ambazo zinafanya shughuli za kibiashara hapa nchini ambazo zimetoa zaidi ya nafasi 100,000 za kazi kwa Watanzania.

Mheshimiwa Kitwanga alitumia fursa ya sherehe hizo kuwahakikishia wawekezaji wote waliopo hapa nchini kuwa Serikali ya Tanzania italinda biashara zao kufuatana na sheria za nchi.

Kuhusu zoezi linaloendelea hapa nchini la kukamata wageni ambao wanaishi na kufanya kazi bila vibali halali alisema kumekuwa na taarifa za uzushi zinazoenezwa hapa nchini na nje ya nchi kuwa Serikali ya Tanzania inawafukuza wageni kwa vile haihitaji raia wa kigeni hapa nchini.

Amesema taarifa hizo ni za uongo zinazolenga kuichafua Tanzania katika jumuiya ya kimataifa na kusema raia wa kigeni wanaokamatwa ni wale tu wasio na vibali halali vya kuishi na kufanya kazi hapa nchini.

Amesema zoezi hilo ni la kawaida na linafanywa kufuatana na Sheria za Uhamiaji lakini halitawahusu wageni wenye vibali halali vya kufanya kazi na kuishi nchini.

Kati ya mwaka 2014 na Januari 2016 Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imetoa vibali vya ukaazi kwa jumla ya wageni 40,765 toka mataifa mbalimbali na idadi hiyo inaendelea kuongezeka siku hadi siku.

Wageni waliofukuzwa kwa sababu mbalimbali mwaka 2015 ni 1,642. Aidha, kati ya 08 Desemba, 2015 na 14 Januari, 2016 raia wa kigeni waliokamatwa kwa kuishi na kufanya kazi nchini bila vibali halali ni kama ifuatavyo:

1.Burundi 284
2.Kenya 26
3.Uganda 13
4.Somalia 7
5.Ethiopia 157
6.DRC 34
7.China 285
8.India 41
9.Zambia 40
10.Nigeria 08
11.Lebanon 01
12.Ivory Coast 10
13.Madagascar 05
14.Malawi 27
15.Korea 09
16.Zimbabwe 01
17.Ghana 01
18.Rwanda 03
19.Afrika Kusini 01
20. Wenye uraia wa utata 11.

Kati ya hawa, wengine wamemepelekwa katika kambi za wakimbizi, hasa raia waliotokea Burundi, wengine wamepewa amri ya kuondoka nchini na wengine kesi zao ziko katika hatua mbalimbali mahakamani.




Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga akizungumza na raia wa China wanaoishi nchini, katika sherehe yao ya kuukaribisha mwaka mpya iliyofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip, jijini Dar es Salaam. Katika hotuba yake, Waziri Kitwanga alisema Tanzania inatambua ushirikiano mzuri wa miaka mingi uliopo kati yake na China, hivyo raia yeyote wa kigeni anatakiwa afuate taratibu za kuishi nchini, na operesheni inayoendelea ya kuwakamata raia wa kigeni, kamwe haitagusa wenye vibali halali.


Kaimu Balozi wa China nchini, Zhang Biao akizungumza katika sherehe ya raia wa China wanaoishi nchini ya kuukaribisha mwaka mpya iliyofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip, jijini Dar es Salaam, kabla ya kumkaribisha Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga (hayupo pichani) kuja kuzungumza na mamia ya wachina hao waliohudhuria sherehe hiyo. Katika hotuba yake, Waziri Kitwanga alisema Tanzania inatambua ushirikiano mzuri, wa miaka mingi uliopo kati yake na China, hivyo raia yeyote wa kigeni anatakiwa afuate taratibu za kuishi Tanzania, na operesheni inayoendelea ya kuwakamata raia wa kigeni nchini, kamwe haitagusa wenye vibali halali.


Raia wa China wanaoishi nchini wakishindana kula Tunda aina ya Tikiti wakati wa Sherehe yao ya kuukaribisha mwaka mpya iliyofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip, jijini Dar es Salaam. Katika Sherehe hiyo ambayo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga (hayupo pichani) alikuwa mgeni rasmi ilihudhuria na mamia ya raia hao wa China. Hata hivyo, Waziri Kitwanga alisema raia yeyote wa kigeni anatakiwa afuate taratibu za kuishi Tanzania, na operesheni inayoendelea ya kuwakamata raia wa kigeni nchini, kamwe haitagusa wenye vibali halali.


Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga akiwapongeza raia wa China walioshinda mchezo wa bahati nasibu walioucheza katika sherehe yao ya kuukaribisha mwaka mpya iliyofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip, jijini Dar es Salaam. Waziri Kitwanga katika hotuba yake alisema nchi yake inatambua ushirikiano mzuri wa miaka mingi uliopo kati yake na China, hivyo raia yeyote wa kigeni anatakiwa afuate taratibu za kuishi nchini, na operesheni inayoendelea ya kuwakamata raia wa kigeni, kamwe haitagusa wenye vibali halali.


Kikundi cha Karate kinachoongozwa na raia wa China wanaoishi nchini kikitoa burudani katika sherehe yao ya kuukaribisha mwaka mpya iliyofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip, jijini Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga (hayupo pichani) ambaye alikuwa mgeni rasmi katika sherehe hiyo, katika hotuba yake alisema nchi yake inatambua ushirikiano mzuri wa miaka mingi uliopo kati yake na China, hivyo raia yeyote wa kigeni anatakiwa afuate taratibu za kuishi nchini, na operesheni inayoendelea ya kuwakamata raia wa kigeni, kamwe haitagusa wenye vibali halali.


Sehemu ya raia wa China wanaoishi nchini, wakimsikiliza kwa makini, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga (hayupo pichani) wakati alipokuwa anatoa hotuba yake kwa Wachina hao katika sherehe yao ya kuukaribisha mwaka mpya iliyofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip, jijini Dar es Salaam jana. Waziri Kitwanga katika hotuba yake alisema nchi yake inatambua ushirikiano mzuri wa miaka mingi uliopo kati yake na China, hivyo raia yeyote wa kigeni anatakiwa afuate taratibu za kuishi nchini, na operesheni inayoendelea ya kuwakamata raia wa kigeni, kamwe haitagusa wenye vibali halali.







(Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi – 24 Januari, 2016)


No comments:

Post a Comment