Monday, December 21, 2015

RAIS MAGUFULI AKUTANA NA MAALIM SEIF IKULU DAR ES SALAAM




TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amekutana naMakamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mgombea Urais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharrif Hamad, leo tarehe 21 Desemba, 2015 Ikulu Jijini Dar es Salaam kufuatia maombi yake ya siku nyingi.

Mazungumzo ya Viongozi hao pia yamehudhuriwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Viongozi hawa kwa pamoja wamejadili hali ya kisiasa Zanzibar na wamefurahishwa na hali ya usalama na utulivu inayoendelea. Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewapongeza Rais wa Zanzibar Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, na viongozi wote wanaoshiriki katika mazungumzo ya kuleta hali ya uelewano Zanzibar.


Rais Magufuli pia amewapongeza na kuwashukuru wananchi wa Zanzibar kwa kudumisha amani na utulivu wakati wa mazungumzo baina ya viongozi wa CUF na CCM yakiendelea huko Zanzibar.

Katika Mazungumzo hayo Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar Maalim Seif Sharrif Hamad amemueleza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania juu ya hali ya siasa Zanzibar kadiri anavyoielewa yeye na Rais Magufuli amemshukuru Makamu huyo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar kwa taarifa yake nzuri huku akimsihi waendelee na mazungumzo hadi suluhisho muafaka lipatikane.

Majadiliano yanayoendelea yanatoa fursa ya kudumishwa kwa utulivu na sifa njema ya nchi yetu. Wote kwa pamoja wamewaomba wananchi waendelee kuwa watulivu ili kutoa nafasi ya majadiliano yanayoendelea kufikia hatma njema. Wameelezea matumaini yao kuwa vyama vya CCM na CUF haviwezi kushindwa kupata suluhu ya mgogoro huo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amemuhakikishia kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano itahakikisha kuwa amani na utulivu unaendelea kudumishwa Zanzibar.


No comments:

Post a Comment