Monday, December 14, 2015

LUKUVI AAHIDI KUKOMBOA MASIKINI BAADA YA KUKABIDHIWA OFISI RASMI



Waziri wa maendeleo ya nyumba na makazi,William Lukuvi amesema atahakikisha wananchi maskini wanapata haki zao za kumiliki ardhi pamoja na kuwawezesha  kuwa na  makazi bora ya kuishi  na kuwashughulikia wale wote wanaotumika kama mawakala na kudhulumu maeneo yao.

 Aidha ametoa siku saba kwa Mkurugenzi wa Wizara hiyo kuainisha utaratibu wa namna ya kuwawezesha wananchi hao kujenga nyumba bora za kuishi la sivyo atambadilisha kazi na kumuweka mtu mwingine ili aweze kutekeleza suala hilo ambalo ni agizo toka kwa Rais.John Magufuli na lipo kwenye ilani yao ya Chama.

 Ameyasema hayo leo alipokuwa akizungumza na Wakuu wa Idara mara baada ya kukabidhiwa rasmi ofisi na Katibu Mkuu wa wizara hiyo,Alphayo Kidata,na kusema kuwa sasa yeye ni mtu mpya ,katika awamu mpya na mambo yake ni mapya hivyo wajipange katika kwenda na kasi yake mpya.
 “Ninataka kumwambia Mkurugenzi wa nyumba na makazi kuwa ilani yetu inataka ujenzi nyumba bora za wananchi na KUWA suala hili haliwezi kufanywa na shirika la nyumba (NHC)pekee,sera yetu inataka kila mwananchi awe na nyumba bora ya kuishi hivyo ifikapo Jumatatu asubuhi nataka kusikia mikakati ya kumuwezesha hata kama ni kwa kupunguzia bei ya vifaa kutokana na kuwa hawawezi kufanya hivyo bila mchago wa Serikali kwani hatuwezi kuvumilia kuona wakiendelea kuishi kwenye nyumba za nyasi,”alisema Lukuvi.
 Pia amesema atahakikisha kuwa kila mwananchi anamilikishwa kipande chake cha ardhi kihalali na kuwa uwezeshaji wao hautawezekana bila kuwa na hati ya umiliki ya ardhi sambamba na kuchunguza ardhi walizopewa wawekezaji kama zimetumika kihalali na kwa matumizi yaliyodhamiriwa au kinyume chake na kuwanyang’anya na pia kuwatayamilikisha maeneo ambayo hayajaendelezwa. “Tutakwenda kuangalia maeneo ya wawekezaji ili kujua kama ardhi walizopewa wamezitumia kwa matumizi waliyoombea au wamezitumia kupata fedha benki na kuzifanyia shughuli nyingine,ninataka kupata taarifa za mashamba na meneo makubwa yaliyofutwa ili tuweze kudhibiti hili,”alisema.
Lukuvi amesema anataka kuwa na chombo katika Wizara yake ambacho kitasaidia katika kudhibiti na kusimamia ujenzi wa nyumba za kibiashara (real estate)kutokana na kumekuwa na watu wengi ambao wamekuwa wakijenga nyumba na kuzipangisha bila kulipia kodi .

Pia amesema kuwa atakutana na watumishi wa Wizara hiyo kutoka idara zote nchini ili kupata taarifa za fedha zilizokusanywa tangu tarehe 1mwezi wa saba tangu pale bajeti ilipoanza na kuwa kwa lengo la kujua jinsi zilivyotumika.  
“Kutakuwa na kikao cha wakuu wa idara wote waliopo hapa na mikoani pamoja na makamishna wa kanda watakuwepo na ninataka nipate taarifa za fedha kuanzia tarehe 1/07mpaka leo yaani fedha mlizopata, mlizokusanya na matumizi yake na pia kazi zilizofanywa na serikali kipindi hicho baada ya bajeti kuanza ,kazi zilizofanywa na wizar hii pamoja na vitengo vyake kote nchini lakini pia nipate taarifa za kila mkuu wa idara malengo yake ya mwaka huu wa fedha yalikuwa yapi na mangapi ameshayatekeleza,”alisema Lukuvi.

“Lakini pia ninataka nipewe utaratibu tuliouweka kuhusu kendeleza fukwe za oysterbay ili wale waliovamia na kujenga maghorofa tujue wanaondoka lini nataka Murugenzi wa mipango miji pamija na manispaa ya kinondoni kunipa taarifa hizo mapema kwani hizo ni fukwe kwa ajili ya wananchi na Rais.Magufuli alishtoa tamko,”alisisitiza.
  Naye Naibu  Waziri wa wizara hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Ilemela,Angela Mabula ,amemshukuru Rais.Magufuli kwa kuwaamini na kuwa watafanya kazi kwa kushirikiana katika kutetea haki za wanyonge na kuhakikisha wanapata haki zao za ardhi na kuwashgulikia watakaohusika na kuwadhulumu bila kujali nafasi zao.
Waziri wa Maendeleo ya Nyumba na Makazi,William Lukuvi akizungumza na wakuu wa Idara mbalimbali leo mara baada ya kukabidhiwa rasmi ofisi na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo,Alphayo Kidata(kulia) na kushoto ni Naibu Waziri Angela Mabulla.


.
                                               


No comments:

Post a Comment