Saa chache baada ya kamati ya Rufani ya shirikisho la kandanda
Tanzania, TFF, chini ya mwenyekiti wake, Wakili Julius Mutabazi Lugaziya
kumrudisha, Michael Richard Wambura kwenye uchaguzi wa Simba sc, mgombea huyo
amesema sasa haki imetendeka na uchaguzi utakuwa wa amani.
Wambura amezungumza na mtandao huu dakika chache zilizopita
na kusema kuwa anaufananisha ushindi wake kama mchezo wa mpira wa miguu.
“Mpira wa miguu una mechi ya nyumbani na ugenini, unaweza
ukafungwa ugenini, ukashinda nyumbani, bila kujali umeshinda goli ngapi, lakini
ninachoweza kusema ni kwamba haki imetendeke, matokeo yametoka, tujipange
kwenda kwenye uchaguzi ili wanasimba wapate viongozi wao wanaowataka” amesema Wambura.
Mgombea huyo ameongeza kuwa hiki sio kipindi tena cha
kutafuta mchawi, bali ni kipindi kinachohitaji wanasimba kuwa makini.
“Ni kipindi cha kuwa makini, kuweka sera zetu hadharani, malengo
yetu hadharani, ili wana Simba wapate fursa ya kuchagua kwa sera, nadhani hilo
ndio ombi langu”.
Ameongeza Wambura. Hata hivyo, Wambura amesema kesho
ataongea na waandishi wa habari makao makuu ya klabu ya Simba mtaa wa Msimbazi,
Kariakoo jijini Dar es salaam.
No comments:
Post a Comment