Friday, March 21, 2014

AMKATA MKEWE KIGANJA, ATUPWA JELA MIAKA 5

Geita

Mkazi wa kijiji cha Bugarama,wilayani Geita, amehukumiwa kwenda jela miaka mitano,baada ya kupatikana na kosa la kumjeruhi mkewe, kutokana na wivu wa mapenzi.

Aliyehukumiwa kutumikia adhabu hiyo, na Mahakama ya Wilaya ya Geita, alitajwa kuwa Musa Lutobeka(30), huku mshitakiwa mwenzake Mashindike Mwanzalima(40) ambaye ni mganga wa jadi akiachiwa huru.

Hukumu hiyo ilisomwa mahakamani hapo juzi, na Hakimu  Zablon Kesase, ambaye alisema ni baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka.

SOMA ZAIDI . . .
''Nimeridhika pasipo kuacha shaka yoyote kuwa mshitakiwa alitenda kosa hili kwa kumkata kiganja cha mkono wa kushoto mwanamke huyu.Hivyo kutokana na kosa la kujeruhi ambalo ni kinyume cha kifungu cha 225 kanuni ya adhabu ya mwaka 2002(RE 2002),natoa adhabu ya kifungo cha miaka mitano jela ili liwe fundisho kwa wengine.''alisema hakimu huyo wakati akisoma hukumu ya kesi hiyo mahakamani hapo.

Kwa upande wake,mwendesha mashitaka wa serikali,Fred Jairo,aliiambia mahakama hiyo kuwa, mshitakiwa alitenda kosa hilo mnamo mwezi Oktoba 9,mwaka jana saa 2 usiku.

Alisema,katika siku hiyo,mshitakiwa alimkata kiganja cha mkono Leah Clement(25) ambaye ni mkewe,na kwamba alipomaliza alitoroka ingawa baadaye alikamatwa akiwa amejificha nyumbani kwa mganga huyo wa jadi.

Alisema,ushahidi ulionesha kuwa mshitakiwa huyo ndiye aliyemkata mkewe kiganja,kutokana na kuwepo hali ya kimapenzi ya kutoelewana,ambapo alimuomba hakimu kutoa adhabu kali kwa mshitakiwa huyo huku ikiomba mshitakiwa wa pili aachiwe huru kwa sababu ya kutokuwepo ushahidi unaomhusisha na tukio hilo.

No comments:

Post a Comment