Monday, January 13, 2014

KAYA 1,426 KUHAMISHWA KISIRI, WENGI WAHOJIWA KISIRI

                                                                   Bunda.

Wananchi kutoka kaya 1426 katika vijiji vitatu vya Nyatwali, Tamao na Serengeti wametoa msimamo wao kwa kuitaka serikali kuweka wazi mpango wa kuhamisha vijiji hivyo na kwamba hawaamini maelezo ya mkuu wa wilaya hiyo, Joshua Mirumbe.

Wamedai kuwa mkuu huyo wa wilaya anahamasisha uwekezaji wa kitalii kwa kujenga makambi ya kitalii katika vijiji hivyo huku akikanusha kuwepo mpango wa kuhamisha vijiji hivyo wakati dalili zinaonekana.

Vyanzo vya habari vimebaini kuwa upo mpango wa vijiji hivyo kuhamishwa kupisha mapito ya wanyama kwenda ziwa Victoria kunywa maji na kuweka makambi ya kitalii.

Vyanzo vilivyofikia gazeti hili vinaeleza kuwa katika kupima mwitikio wa wakazi wa vijiji hivyo Desemba 16 na 31 mwaka jana baadhi ya maofisa kutoka TANAPA, ofisi ya mkuu wa mkoa, ofisi ya mkuu wa wilaya, ardhi, mazingira na mali asili walikutana na wawakilishi kutoka vijiji hivyo katika Hoteli ya Kilipark mjini Bunda.

Wawakilishi hao walikuwa ni watu maarufu na wenyeviti wa serikali ya vijiji hivyo ambapo kila mtu kwa wakati wake aliitwa ndani ya ukumbi na kuhojiwa kuhusu hatua ya kuwahamisha wananchi katika vijiji hivyo.

“kweli tuliitwa pale na kila mtu alikuwa anaingia mmoja mmoja…..mimi zamu yangu ilipofika niliitwa kwa jina na nilipoingia ndani ya ukumbi nilikuta watu sita, wawili walijitambulisha kuwa wanatoka TANAPA…” kilisema chanzo hicho na kuongezea,

“alikuwepo ofisa kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa wa Mara…..hawa wa TANAPA na ofisi ya mkuu wa mkoa sikuwakariri majina lakini wale waliotoka hapa wilayani katika ofisi ya mkuu wa wilaya, ardhi, mazingira na mali asili nawafahamu(majina tunahifadhi)”

“baada ya maelezo mengi yaliyolenga kutushawishi kukubali kuhama mwishoni walituambia turudi vijijini kuwashawishi wananchi wakubali kuhama” kilieleza na kuongezea.

“nilipohoji sababu ya wananchi kuhamishwa walisema eneo la vijiji hivyo tangu mwaka 1974 vilikuwa ni mapito ya wanyama kwenda Ziwani na vilitengwa rasmi kisheria iliyosainiwa na rais wa kwanza hayati Mwalimu Nyerere na kwamba sasa imefika wakati wananchi kupisha” kilisema chanzo.

Kwa mujibu wa chanzo hicho wakazi wa vijiji hivyo walitakiwa kujiandaa kuhama Julai mwaka huu na kwamba watakaokubali watalipwa fidia.

Pia utafiti umebaini kuwa fukuto la kutaka kuhamishwa kwa vijiji hivyo iliibuka mwaka 2002 ambapo mkuu wa wilaya ya Bunda kwa wakati huo Bi. Hawa Mchopa hakukubaliana nalo.

Katika ushauri wake Mchopa aliiomba serikali kuweka uzio kati ya wananchi na mapito hayo ya wanyama ili kuwapa njia rahisi ya kutowaingilia wananchi na kwamba serikali ingechimba mabwawa ndani ya hifadhi ya Serengeti kupunguza uhaba wa maji kwa wanyama hao.

Mwishoni mwa wiki hii viongozi wa vijiji hivyo vitatu viliitisha mkutano wa adhara na kutoa msimamo wao kwamba kama Serikali na TANAPA ina mpango wa kuwahamisha wananchi wao hawako tayari.

Katika mkutano wa adhara wa Kijiji cha Nyatwali uliomalizika jana muda mfupi tunaingia mtamboni Mwenyekiti wa Kijiji hicho Jumanne Watema kwa niaba ya wananchi walimtaka mkuu wa mkoa wa Mara kufika katika vijiji hivyo kuzungumza na wananchi kuhusu sakata hilo.
Kuhusu ujenzi wa makambi ya kitalii wananchi hao walisema ni jukumu la mwekezaji kufika kijijini na kuingia mkataba na wananchi na sio viongozi wa ngazi ya juu.

Wananchi hao pia wanaungwa mkono na mbunge wa jimbo la Bunda Stephen Wassira.

Baada ya gazeti hili kuibua mpango wa wananchi hao kutaka kuhamishwa Januari 6 mwaka huu mkuu wa wilaya ya Bunda Joshua Mirumbe aliitisha kikao cha kamati ya serikali za vijiji hivyo vitatu na kukanusha mpango wa kuhamisha vijiji hivyo.

Hata hivyo katika mikutano ya adhara iliyokaa mwishoni mwa wiki wananchi hao waliomba mkuu wa wilaya na mkuuwa mkoa wa Mara kufika kijijini hapo na kuzungumza na wananchi katika mkutano wa adhara kuhusu sakata hilo.



No comments:

Post a Comment