Friday, August 02, 2013

SIMBA KESHO KIKOSI CHAKE HADHARANI

KLABU ya Simba kesho inashuka uwanjani kucheza mchezo wa kirafiki na timu ya Kombani ya Jeshi la Polisi utakaopigwa kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mchezo huo ni maandalizi kwa timu ya Simba ambayo inatarajia kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao wa 2013-14 utakaoanza Agosti 24 katika viwanja tofauti nchini.

Kwa upande wa Kombaini ya Polisi inajiandaa na mashindano ya kimataifa ya nchi za SADEC yatakayofanyika nchini Namibia mabayo yataanza Agosti 16-30.


Akizungumzia mchezo huo Ofisa Habari wa Simba Ezekiel Kamwaga alisema timu yake itautumia kwa ajili ya kuwatangaza wachezaji wake wapya.

Kamwaga alisema kwa sasa kikosi chao kimekamilika hasa baada ya kumalizana na mabeki wawili wa kigemi ambao wametua nchini jana.

"Leo (jana) wachezaji wetu wawili ambao wote wanacheza nafasi ya beki wanakuja, Owino (George) kutoka Uganda na Kaze (Girbert) kutoka Burundi, tukimalizana nao mapema pia watacheza jumamosi", alisema.

Kamwaga aliongeza kuwa wachezaji hao wote wawili wanasajiliwa ili kumaliza tatizo la muda mrefu wa beki wa kati ambalo lilikumba timu hiyo kwa muda mrefu.

"Kuelekea katika siku ya Simba marifu kama Simba Day tutacheza jumamosi na Kombaini ya Polisi, tunaomba mashabiki wetu wajitokeze kwa wingi kuja kuangalia kikosi chao kamili cha Simba kwa ajili ya msimu ujao," alisema.

Kwa upande wake Ofisa wa Michezo wa jeshi la Polisi SSP Jonas Mahanga alisema timu zote zitapata mazoezi ya kutosha kwa kuwa zinaundwa na wachezaji wenye uwezo wa hali juu.

Akiizungumzia timu yake ambayo inaundwa na mastaa kutoka katika timu mbalimbali za jeshi alisema Simba watarajie kupata upinzani mkali kutoka kwa timu hiyo.

"Naamini Simba watapata mazoezi ya kutosha kutoka kwetu, timu yetu inaundwa na wachezaji kutoka Tanzania Bara na Zanzibar ambao wanacheza katika timu zetu za polisi, hivyo naamini utakuwa mchezo mzuri," alisema.

Afande Jonas kama ambavyo anajulikna zaidi akizidi kufananua juu ya mchezo huo alidai kuwa mashabiki wa timu zote wafike kwa wingi kwa ajili ya kushuhudia mchezo huo.

Kwa upande wake Mratibu wa mchezo huo Geogre Wakuganda alisema mandalizi kwa ajili ya mchezo huo yamekamilika kwa asilimia kubwa.

Wakuganda aliongeza kuwa dhumuni la mchezo huo ni kwa ajili ya kuzipa mazoezi timu hizo ambazo zinashiriki mashindano tofauti.

"Hii ni kawaida kila mwaka inapofikia wkati kama huu ambao timu zinakuwa zinajiandaa na ligi huwa tunaziletea timu kwa ajili ya kuzipa mazoezi, Simba ilicheza na URA ya Uganda na sasa itacheza na Polisi Jumamosi," alisema.

Wakuganda alivitaja viingilio katika mchezo huo kwa upande wa VIP A ni 20, 000 VIP B 15,000, VIP C 10,000 na mzunguko ni 5,000.



No comments:

Post a Comment