Shinyanga
Mwanamke mwingine mkazi wa Lubaga Manispaa ya Shinyanga amenusurika kifo kutokana na kipigo alichokipata kutoka mumewe akimtuhumu kutopokea simu haraka. Kipigo hicho kilisababisha mwanamke huyo kulazwa hospitali akiwa mahututi mwishoni mwa wiki iliyopita.
Kwa mujibu wa maelezo ya mwanamke huyo (jina limehifadhiwa) ambaye hivi sasa amelazwa katika hospitali ya serikali mkoani Shinyanga akipatiwa matibabu chanzo cha yeye kupokea kipigo kutoka kwa mumewe ni kuchelewa kupokea simu aliyokuwa amempigia.
Mwanamke huyo amemtaja mumewe kuwa ni Daniel Daud na kwamba tukio hilo lilitokea wiki iliyopita baada ya kushindwa kupokea simu aliyopigiwa na mumewe kutokana na wakati huo alikuwa akivuka barabara na hivyo kuhofia kugongwa na gari.
Alisema mara ya kufika nyumbani mumewe alianza kumfokea na kuhoji kwa nini alichelewa kupokea simu aliyokuwa amempigia na kudai huenda alikuwa na mwanamume mwingine na ghafla alianza kumshambulia kwa kipigo sehemu mbalimbali za mwili wake.
“Nilijaribu kumuelewesha mume wangu kwamba wakati akipiga simu nilikuwa navuka barabara hivyo nisingeweza kupokea simu wakati huo nikihofia kugongwa magari, na kwamba hata angemuuliza dada yake mdogo mwenye umri wa miaka saba tuliyekuwa pamoja angemthibitishia ukweli,”
“Pamoja na maelezo yangu hakunielewa, hata dada yake alipojaribu kunitetea na kueleza ukweli bado aliendelea kunifokea na kudai mimi ni mwanamke malaya na hivyo alianza kunipiga ngumi sehemu mbalimbali za mwili na kunisababishia maumivu makali mwilini,” alieleza.
Hata hivyo alisema pamoja na juhudi za wifi yake kutaka kuamua ugomvi huo hakufanikiwa kutokana na kuwa mdogo kiumri ambapo baada ya kipigo alichukua uamuzi wa kumfungia chumbani na kisha yeye mwenyewe aliondoka nyumbani na kutokomea kusikojulikana.
Alisema alikaa ndani bila ya matibabu yoyote na kusababisha sehemu zilizokuwa na majeraha kuanza kutoka usaha huku akihisi maumivu makali na kwamba aliokolewa katika hali hiyo na jirani yake aliyekwenda kumuangalia baada ya kutomuona akitoka nje kwa siku mbili.
“Rafiki yangu mmoja alikuja nyumbani wakati mume wangu hayupo nilimweleza hali yangu kuwa si nzuri kutokana na kipigo nilichokipata, alisikitika sana na kuchukua uamuzi wa kuniiba ambapo alitafuta gari na kunikimbiza hapa hospitali ili niweze kutibiwa baada ya kupata fomu namba tatu kutoka polisi,” alieleza.
Kwa upande wake mganga mfawidhi katika hospitali ya serikali mkoani Shinyanga, Dkt. Fredrikck Mlekwa alithibitisha kupokelewa kwa mgonjwa huyo hospitalini hapo na kwamba hivi sasa amelazwa wodi namba saba ambayo ni ya majeruhi akiendelea kutibiwa majeraha aliyoyapata kutokana na kipigo cha mumewe.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Evarist Mangala amekiri kutokea kwa tukio hilo na kwamba hivi sasa polisi inaendelea na msako wa kumtafuta mtuhumiwa huyo ili aweze kukamatwa na kufikishwa mahakamani kujibu shitaka la shambulio la kudhuru mwili alilomtendea mkewe.
Tukio hili ni la pili kutokea mjini Shinyanga ndani ya wiki moja likihusiana na vitendo vya kikatili vinavyofanywa na baadhi ya wanaume dhidi ya wake zao ambapo tukio la awali lilitokea huko katika Mtaa wa Katunda baada ya mwanamke mmoja aliyedai talaka kupokea kipigo kikali kutoka kwa mumewe.
No comments:
Post a Comment